MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema, wamekusanya Shilingi Bilioni 991, jambo ambalo linaendelea kuimarisha mfuko huo.
Dkt. Mduma alisema hayo wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari, jijini Dar es Salaam, kwenye Mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) kwa ajili ya kuelezea mafanikio yaliyopatikana wa kipindi cha Miaka 10 tangu mfuko huo ulipoanzishwa na miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema, mbali na makusanyo hayo, thamani ya mfuko imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 445 wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani, hadi Shilingi Bilioni 748 ambapo, thamani ya mfuko huo inatarajiwa kufikia Shilingi Bilioni 766.6 katika mwisho wa mwaka 2024/2025 wakati.

Alisema, mbali na ukuaji wa mfuko, pia wameboresha mifumo ya ushughulikiaji wa fidia kwa wafanyakazi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, ambapo sasa zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinazotolewa na WCF, zinapatikana mtandaoni “Hatua hii imeongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa mfuko.”
“Hili linashuhudiwa wakati ambao kumefanyika mabadiliko ya kisera kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa na mfuko, huku moja ya eneo lililoguswa ni kushusha ada za uchangiaji katika mfuko kwa watu wa sekta binafsi; kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 ya mapato ya kila mwezi ya wafanyakazi wao.
“Uamuzi huu umefanya taasisi binafsi kuchangia sawa na taasisi za umma na lengo ni kumpunguzia mzigo mwajiri ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia, sasa azielekeze kwenye maeneo mengine ya uendeshaji na uzalishaji.
“Hilo limechangia kuongeza usajili wa waajiri kwa mwaka kutoka 2,289 mwaka 2020/21 mpaka waajiri 4,136 idadi ambayo ilipelekea kufikia jumla ya waajiri 38,512 waliopo ndani ya mfuko huo sasa.
Hii ni kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba,” alisema Dkt. Mduma.

Aidha, Dkt. Mduma alisema, tathmini iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha WCF kuwa imara kwa miaka 30 ijayo.
“Wataalam wa Kimataifa waliotupima walithibitisha kuwa tunakidhi viwango vya ubora. Hii inajenga imani kwa wadau wetu kuwa tumejidhatiti kutoa huduma zenye viwango vya hali ya juu. Kila mwaka wataendelea kutufanyia tathmini kuhakikisha tunazingatia viwango hivyo,” alisema.
Aliendelea kusema, mfuko huo umefanya mabadiliko makubwa ikiwemo kufuta madai ambayo walikuwa wanadai kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi waliochelewesha kuwasilisha michango yao kwa wakati.
Dkt. Mduma alisema, kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, kabla ya mabadiliko ya sheria, WCF ilikuwa ikitoza riba ya asilimia 10 kwa mwezi kwa michango iliyocheleweshwa, hali ambayo ilisababisha ongezeko kubwa la deni kwa waajiri.
“Busara ilitumika katika Awamu ya Sita ambapo riba hiyo kubwa ilifutwa, na kubaki deni la msingi tu. Waajiri waliotakiwa kulipa walipewa msisitizo kulipa deni hilo la msingi pekee,” alisema.