Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nishati January Makamba amesema, katika kukabiliana na changamoto ya kusuasua kwa miradi ya kusambaza umeme inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuanzia sasa Wizara yake itabadilisha taratibu za upatikanaji wa zabuni, na kuongeza nguvu ya usimamizi wa miradi hiyo kwa lengo la kuwabana wakandarasi wanaochelewa kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa.
Alisema hayo kwenye hafla ya kusaini mikataba na wakandarasi wa Kampuni nne ambazo zimepewa jukumu la kusambaza umeme kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji kupitia mradi wa PERI Urban III, iliyofanyika leo Disemba 19,2022 kwenye kituo cha mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyarere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
Kampuni ambazo zimesaini mikataba hiyo ambayo itatekelezwa kwenye mikoa ya Geita, Mtwara, Mbeya, Tabora, Tanga Singida na Kigoma, ni Central Electricals International Ltd, DERM Electrics (T) Ltd, OK Electrical & Electronics Services Ltd na DIEYNEM Co Ltd.
Waziri Makamba alisema, fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umeme ni nyingi, lakini kasi ya wakandarasi sio ya kuridhisha, hivyo kuna haja ya kuwabana zaidi wakandarasi hao ili kuchochea kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Kuna kusuasua katika utekelezaji wa miradi ya umeme kwenye mikoa yote, fedha zinapelekwa nyingi, ila wananchi hawaoni kasi; wakandarasi wanachimba mashimo wanaondoka, wanaweka nguzo na waya wanaondoka, hatuwezi kuendelea hivi,” alisema Waziri Makamba.
Alisema, kabla ya kuingia mwaka mpya 2023, watakuwa wamekamilisha suala la ajira kwa waratibu wa kusimamia miradi ya REA ambao watakuwa kwenye Wilaya na Mikoa yote nchini.
“Tumepata kibali, tutaajiri waratibu wa miradi ya REA vijana 130 ambao watakuwepo kwenye kila Mkoa na Wilaya, ambao kila kukicha watakuwa vijijini kuwasimamia wakandarasi na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya miradi inayotekelezwa,” alisema.
Aidha, Waziri Makamba alisema, wataweka utaratibu mzuri wa waratibu hao kutoa taarifa kwa haraka kwa kila kinachojiri kwenye miradi hiyo ikiwemo utendaji wa wakandarasi, huku akisisitiza kwamba kuanzia sasa watawapima wakandarasi kwa utendaji wao na wote ambao wanasuasua kwenye miradi ambayo wanaendelea kuitekeleza hivi sasa, hawatapata nafasi ya kutekeleza miradi mingine.
“Nawaambia wakandarasi, kuanzia sasa tutabadilisha masharti ya utoaji wa zabuni; kama kazi unafanya kwa kusuasasua hivi sasa na upo nyuma ya ratiba, sahau kupata kazi nyingine, kama umemaliza mradi na ulitusumbua, usiombe mradi mwingine,” alisisitiza Makamba na kuongeza kuwa, ni bora wabaki na wakandarasi wachache kuliko wengi ambao hawafanyi vizuri.
Katika hatua nyingine, Waziri Makamba alisitisha zoezi la kusaini mkataba kwa Kampuni ya ETDCo ambayo ilishinda zabuni ya usambazaji umeme kwenye mikoa ya Geita na Kigoma na kuwataka wamalize kazi ya kusambaza umeme kwenye mikoa ya Mbeya na Katavi.
“Mtu ana asilimia 35 ya utekelezaji wa mradi, halafu anaomba kazi mpya, ETDCo wana kazi Mbeya, wanayo kazi nyingine Katavi ambayo imefikia asilimia 41%, wamalize kwanza kazi wanayoendelea nayo, leo hakuna kusaini mkataba wa Mradi wa PERI Urban III,” alisisitiza Waziri Makamba.
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi Hassan Saidy aliwataka wakandarasi hao ambao wamesaini mikataba kutambua kwamba, miradi wanayokwenda kutekeleza ina malengo maalum, hivyo wanapaswa kuwa waadilifu.
Mhandisi Saidy alisema, lengo la Serikali ni kutatua kero ya ukosefu wa umeme kwa watanzania, “hii ni miradi ya Serikali, hivyo wakandarasi wanapaswa kwenda kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa Serikali kwenye maeneo wanayotekeleza miradi,”
Alisema, watawatambulisha wakandarasi hao kwa wakuu wa Mikoa na Wilaya, huku akiwataka kuwashirikisha viongozi wa Mitaa, kutumia vifaa vyenye ubora katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuzingatia usalama wafanyakazi wao.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi waliotia saini mikataba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya O.K. Electrical & Electronics Services Ltd, Mrisho Masoud alisema, watafanyia kazi nasaha zilizotolewa na Waziri January Makamba.
Mrisho aliwataka wakandarasi wenzake kutofanya mzaha kwani wameaminiwa, hivyo wanapaswa kwenda kufanya kazi na kutimiza wajibu wao ili miradi hiyo “tutende haki kwa kumaliza miradi hii kwa wakati, Mheshimiwa Waziri tumesikia nasaha zako, tutazifanyia kazi.”