Majaribio ya kichwa cha Treni SGR yanaridhisha

0

Na Jumbe Abdallah

WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amefanya ziara fupi ya kuona majaribio ya kichwa cha treni ya umeme cha Reli ya kiwango cha Kimataifa – SGR kilichopo kwenye Stesheni ya Pugu jijini Dar es Salaam na kuridishwa na majaribio hayo.

Prof. Mbarawa alisema, lengo ni kuona uwezo wa ufanyaji kazi wa kichwa cha umeme cha SGR ambapo hivi sasa kipo kwenye majaribio mbalimbali.

“Majaribio ya kwanza yanafanyika kama majaribio ya mifumo ya breki, mifumo ya breki za umeme na upepo na mwendokasi wa Kilomita 160, nimeridhika kwamba kichwa kizuri na kina uwezo mkubwa” alisema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameeleza kuwa kichwa hicho ni moja kati ya vichwa 17 ambavyo Serikali imenunua kutoka nchini Korea Kusini vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 254 za kitanzania ambapo vichwa vingine vitatu vinatarajiwa kufika mwishoni mwa mwezi Disemba.

“Baada ya majaribio haya, majaribio ya pili yanayofuata ni kukifunga kichwa hiki na mabehewa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro” alisema Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amewasihi wananchi kuendelea kuwa na subra na punde majaribio yatakapokamilika na kujiridhisha kuanza kwa safari za abiria na mizigo hakika wananchi watafaidi matunda ya SGR.

SGR itatoa fursa na kurahisisha maisha ya watanzania kwa kutumia mwendokasi wa Kilomita 160 kwa saa ambapo itatumia mwendo wa saa moja na nusu kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na masaa matatu Dar es Salaam hadi Dodoma pamoja na mwendo wa saa saba kutoka Dar es Salam hafi Mwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here