Majaliwa: Nimeridhishwa na maandalizi ya maadhimisho ya Mei Mosi

0
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema, ameridhishwa na maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo yatafanyika kitaifa mkoani Arusha.

Alisema hayo leo (Jumanne, Aprili 30, 2024) wakati akikagua maandalizi hayo ambayo yatafanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jijini Arusha.

“Nimeridhishwa na maandalizi, niwatie shime tukamilishe sehemu iliyobaki, kesho tutakuwa wote, Waziri Deogratius Ndejembi yupo na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo hapa”

Majaliwa alisema, Serikali inaridhishwa na ushirikiano uliopo baina yake na vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kuwajibika kwa yote muhimu yanayowaguswa wafanyakazi “tunazungumza pamoja na kukiwa na jambo lolote tunashirikishana, muelekeo wetu bado ni mzuri”

Kwa upande wake, rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA),Tumaini Nyamhokya ambaye alikuwepo katika maandalizi hayo alisema, kamati za maandalizi zimefanya kazi kubwa ikiwemo hamasa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo. “Mpaka sasa maandalizi yote yamefikia asilimia 95, na hizo tano kwa Saa machache zilizobaki tunakwenda kuyamaliza”

Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here