Achangisha zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6 katika harambee ya Mei Mosi 2025
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yana lengo la kuhamasisha utoaji wa haki za wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi kwa ujumla.
Majaliwa ameyasema hayo jana usiku, Aprili 5, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharamia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Singida.
Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.
Alisema, dhumuni jingine la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi michango ya wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na uchumi, Mei Mosi ni fursa ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi duniani kote.
Waziri Mkuu alisema, mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo jumla ya Shilingi Bilioni 1.62 zilikusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslimu, lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi Milioni 832.8.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, rais wa TUCTA, Tumaini Nyamuhokya, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata.