Mahakama Kuu wapambana kumaliza mlundikano wa mashauri

0
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Agnes Mgeyekwa akizungumza na Watumishi wa Mahakama hiyo (hawapo katika picha) katika kikao cha Watumishi kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Shule ya Sheria 'Law School' jijini Dar es Salaam.

Na Mary Gwera, Mahakama

MAHAKAMA ya Tanzania inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha inatekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la utoaji haki sambamba na kufikia kwa vitendo Dira yake ya Utoaji Haki Sawa kwa wote na kwa wakati.

Jitihada hizi zinadhihirishwa na kasi ya uondoshaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali za Mahakama nchini ikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania mojawapo ikiwa ni Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi.

Katika kikao cha Watumishi wa Divisheni hiyo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Shule ya Sheria ‘Law School’ jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Agnes Mgeyekwa amewapongeza watumishi wa Divisheni hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ulioiwezesha Mahakama hiyo kuondosha jumla ya mashauri 2249 kwa kipindi cha mwezi Februari 2022 hadi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na Watumishi wa Divisheni hiyo, Mgeyekwa alisema idadi hiyo inajumuisha jumla ya mashauri ya mlundikano 167 yaliyovuka mwaka 2021.

“Kila mtumishi amekuwa na mchango mkubwa sana kwa sababu kazi ya kuondosha mashauri sio kwa Majaji peke yao, bali kila mtumishi. Hivyo, pongezi za takwimu nzuri za uondoshaji mashauri zinakwenda kwa kila mtumishi wa Divisheni hii,’ alisema.

Alisema, katika kipindi hicho cha Februari hadi Oktoba mwaka huu mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa 1684, yaliyoamuliwa 2249 na yanayoendelea (pending) ni 1014.

Aidha, Mgeyekwa alibainisha kuwa, hadi kufikia Novemba 4, 2022 mashauri ya mlundikano yaliyosalia katika Divisheni hiyo ni 46 pekee huku 12 kati ya hayo yapo nje ya uwezo wa Mahakama hiyo kwa sababu kuna mashauri ya rufaa yanaendelea Mahakama ya Rufani na sababu nyingine ni kutolewa kwa amri za kutoendelea kuyasikiliza kutoka Mahakama ya Rufani. “mkakati uliopo ni kumaliza mashauri 34 kabla ya mwisho wa mwaka huu.”

Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, Divisheni ya Ardhi imefanya jitihada mbalimbali zenye lengo la kuondosha mashauri mojawapo ikiwa ni pamoja na kutumia vikao maalum vya kuendesha mashauri ‘sessions’ ambapo mashauri 59 yalipangiwa mbele ya Majaji watano (5) kutoka nje ya Kituo, kati ya hayo mashauri 51 yalimalizika, saba (7) yanaendelea kusikilizwa na shauri moja (1) linasubiri hukumu.

“Divisheni imeweka kipaumbele cha kibajeti kwenye kuondosha mashauri hasa ya mlundikano ili kufikia malengo iliyojiwekea ambapo walilazimika kualika Majaji na Naibu Wasajili kutoka vituo vingine ili kuongeza nguvu zaidi ya kuondosha mashauri hayo,” alisisitiza Jaji Mfawidhi.

“Mbinu hii yenye matokeo chanya huongeza matumizi ya bajeti, kwa kuwa mashauri ndiyo jukumu la msingi la Mahakama, Menejimenti imeona ni busara kujikita kwenye matumizi hayo, ambapo tulialika Majaji na Naibu Wasajili walioendesha vikao vya Mahakama ‘session’ na kuiwezesha Divisheni kung’ara na hivyo watumishi wote mnastahili kujipongeza na kuona fahari,” alisema Mgeyekwa.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Majaji na Watumishi wote wa Divisheni hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2020/2021 hadi 2024/2025.

Mtaalam Mwezeshaji wa mada hii alikuwa Kisingi Mhando, Mchumi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu vipengele muhimu vya Mpango Mkakati huo na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake.

Mada nyingine iliyowasilishwa na Mwezeshaji, Betty Jones ilihusu Mbinu za Kukabiliana na Msongo wa Mawazo (Stress Management) katika maisha ya kila siku nje na mahali pa kazi ili kuwajengea watumishi uwezo na mbinu za kumudu msongo ‘stress’ na kutimiza malengo ya Taasisi.

Kadhalika, Mada nyingine iliyowasilishwa ilihusu Mpango wa Bajeti ya Divisheni, Usimamizi na Matumizi yake kwa Mwaka 2022/23 iliwasilishwa na Peter Mbaguli, Afisa Tawala akishirikiana na Hawa Wanguvu, Afisa Hesabu Mwandamizi.

Katika majadiliano ya pamoja watumishi walitoa hoja zilizolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kuongeza idadi ya watumishi, vitendea kazi, vikao vya watumishi wote pamoja na kuboresha masilahi ya watumishi ili kuwapunguzia ukali wa maisha.

Katika ufafanuzi wa hoja hizo, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Anatory Kagaruki alisema, masuala yote yanazingatiwa kikamilifu huku na kuongeza kuwa, uwezo na mipango ya kibajeti katika ngazi ya Taasisi na Divisheni ndiyo unaotoa dira ya namna ya kutimiza mahitaji hayo.

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Watumishi wenzangu kwa kuchapa kazi, hata hivyo tusisahau vipaumbele vyetu ambavyo ni kuendelea na matumizi ya TEHAMA, kuimarisha ushirikiano na wadau na nidhamu kwa watumishi,” alisema Kagaruki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here