MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza rasmi kushuka kwa bei za mafuta, ambapo bei mpya zinatarajiwa kuanza kutumika kuanzia kesho, Oktoba 9, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa ZURA, Mbarak Hassan Haji huko ofisini kwao zura Maisara wilaya ya mjini.
Amesema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo Wastani wa mwenendo wa Mabadiliko ya bei za mafuta Duniani, Gharama za uingizaji wa Mafuta katika Bandari ya Tanga, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta, Gharama za Usafiri, Bima na ‘Preminium’ hadi Zanzibar, Kodi za Tozo za Serikali na Kiwango cha faida kwa Wauzaji wa Jumla na Reja Reja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei mpya kwa bidhaa za mafuta zitakuwa mwezi huu ni Petroli, TZS 2,809 kwa lita kutoka TZS 2,943, Dizeli, TZS 2,944 kwa lita kutoka TZS 2,993, Mafuta ya Ndege TZS 2,343 kwa lita kutoka TZS 2,502 na Mafuta ya taa yatabaki kwa bei ileile ya TZS 3,000 kwa lita kwa mwezi huu wa Oktoba.
Aidha amesema Sababu za mabadiliko ya Bei za Mafuta kwa Mwezi Oktoba, 2025 zinatokana na mabadiliko ya bei za ununuzi katika soko la dunia, gharama za uingizaji wa bidhaa za mafuta kutoka soko la dunia hadi kufika Zanzibar pamoja na Fedha za kigeni.
Mamlaka inawahimiza Wananchi kununua Mafuta katika Vituo halali vya kuuzia Mafuta na kudai Risiti za Kielectroniki kila wanaponunua mafuta hayo ili zinapotokezea changamoto zozote wapate kusaidiwa.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) hutangaza bei hizo za Mafuta kila ifikapo tarehe 8 ya kila mwezi.