Maduro: Vita vya uchumi ni jinai dhidi ya binadamu

0
FILE PHOTO: Venezuelan President Nicolas Maduro in Caracas, Venezuela, December 8, 2020. REUTERS/Manaure Quintero/File Photo

Caracas, VENEZUELA

RAIS Nicolas Maduro wa Venezuela amesema, vita vya kiuchumi vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi yake ni jinai dhidi ya binadamu na ametabiri kuundwa ulimwengu wa kambi kadhaa kwa mchango wa Iran, Russia na China.

Hali mbaya ya kiuchumi iliyosababishwa na vikwazo vya Marekani imeathiri uchumi wa Venezuela ambayo ni nchi yenye utajiri mkubwa zaidi katika eneo la Amerika Kusini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Maduro amekosoa vikali kuendelezwa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Venezuela, katika barua yake kwa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambayo imesomwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Carlos Faria.

Katika barua yake hiyo, rais wa Venezuela amelaani kutekelezwa ‘vikwazo haramu 913’ dhidi ya nchi yake na kusisitiza kwa kusema: “hatua za mabavu na za upande mmoja zinazoandamana na ukoseshaji na uchokozi wa kimfumo zinayabana maisha na haki za pamoja za nchi yangu na zinazidisha mateso ya watu; na kwa sababu hiyo hatusiti kulaani vitendo hivi vya kidhalimu ambavyo ni sawa na jinai dhidi ya binadamu”.

Rais wa Venezuela amekadiria hasara iliyosababishwa na vikwazo vya miaka ya karibuni vya Magharibi dhidi ya Venezuela kuwa ni takriban Dola Bilioni 150 na akazikosoa Ulaya na Marekani kwa kuiba tani 31 za dhahabu zilizowekwa katika benki ya Uingereza zenye thamani ya Dola Bilioni 1.3.

Barua ya Nicolas Maduro imeeleza kuwa, pamoja na uhasama na uadui wote huo waliofanyiwa, wananchi wa Venezuela hawajasalimu amri bali wamejitengenezea njia ya kuimarisha amani ya kijamii, kuboresha uchumi wao na kuimarisha demokrasia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here