Na Mohamed Saif
MABALOZI wa Umoja wa Ulaya wameridhishwa na ubora na kasi ya ujenzi wa mradi wa shilingi bilioni 69 wa Dakio jipya la Maji katika eneo la Butimba Jijini Mwanza.
Mabalozi wa Umoja huo wamepongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji kote Nchini za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya majisafi na salama.
Ujumbe huo wa Mabalozi wa Nchi za Umoja wa Ulaya umehusisha Waheshimiwa Mabalozi kutoka Umoja wa Ulaya, Ubelgiji, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Spain na Poland ambao ulitembelea Mradi wa Maji wa Butimba Januari 24, 2023.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfredo Fanti alisema ujumbe alioambatana nao umeridhishwa na hali waliyoishuhudia ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Butimba.
“Mradi wa Maji wa Butimba ni miongoni mwa miradi inayojengwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na baadhi ya Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya; kwa pamoja tumeridhishwa na tumefurahishwa na tuliyoyashuhudia, mradi unakwenda vizuri na ujenzi wake unazingatia ubora, tunaimani utakamilika kwa wakati na hivyo kupunguza adha ya maji kwa wakazi wa Mwanza,” alisema Balozi Fanti.
Balozi Fanti alisema, ujumbe huo umefurahishwa na jitihada za makusudi za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwasogezea huduma za kijamii na kuwaletea maendeleo wananchi wake na ameahidi kuwa Umoja wa Ulaya unaendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza na Ujumbe huo ofisini kwake, alifikisha salama za shukrani kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na wananchi wa Mwanza kwa ujumbe huo kwa ushirikiano na sapoti wanayoitoa kwa maendeleo ya wananchi.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba ya wananchi wa Mwanza ninaomba mpokee shukrani zetu za dhati kwa ushirikiano mnaoendelea kutupatia kwa maslahi mapana ya kuimarisha ustawi wa Watanzania wote,” alisema Malima.
Aidha, akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe huo kwenye mradi wa maji wa Butimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele alisema amefurahishwa na namna ambavyo ujumbe huo umeridhishwa na utekelezaji wa Mradi.
“Tunajivunia kupokea ugeni huu kwenye miradi yetu hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya miradi ikiwemo huu wa Butimba unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya kupitia mkopo wa masharti nafuu,” alisema Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kukahikisha anatafuta fedha za kujenga miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa miradi ya maji.
“Tunamshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa namna ambavyo anachukua hatua stahiki za kuhakikisha miradi inatelekezwa kwa wakati na tunamshukuru kwa kutuunganisha na wadau mbalimbali ikiwemo Nchi za Umoja wa Ulaya ambao wanasaidia kuendeleza miradi,” alisema Mhandisi Msenyele.
Alisema, kwa sasa mradi wa Maji wa Butimba umefikia asilimia 65 na kwamba matarajio ifikapo mwishoni mwa Mwezi Aprili mwaka huu majaribio ya mradi yataanza na kwamba hadi kufika Mwezi Juni mradi utakuwa umefikisha huduma ya maji kwenye maeneo yanayokusudiwa.