BRASILIA, Brazil
RAIS wa zamani wa Brazil Luiz InĂ¡cio Lula da Silva Jumapili alimshinda Jair Bolsonaro katika uchaguzi ambao unaashiria kurejea madarakani kwa kishindo kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto.
Lula da Silva alikuwa na asilimia 50.8 ya kura ikilinganishwa na asilimia 49.2 ya kura za Bolsonaro baada ya asilimia 99.1 ya kura kuhesabiwa na kwa msingi huo Mahakama ya Juu ya Uchaguzi ikasema ilitosha kumtangaza mshindi.
Ushindi wa kiongozi huyo umetajwa kuwa ni kemeo kwa sera za mrengo wa kulia ambazo Bolsonaro alikuwa akitekeleza, ambapo Rais huyo aliyemaliza muda wake analaumiwa kwa kuvuruga uchumi wa Brazi.
Pia, Bolsonaro analaumiwa kwa usimamizi mbovu wa sekta ya afya, jambo ambalo lilisababisha nchi hiyo kuongoza duniani kwa idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na janga la COVID-19.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Lula da Silva alisema, Brazil sasa imerejea tena katika uga wa Kimataifa na haitakuwa nchi iliyotengwa.
Lula da Silva alisema, atarejesha sera za kustawisha ukuaji wa uchumi ambazo zilisaidia kuwaondoa Mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini wakati alipoitawala Brazil kutoka 2003 hadi 2010.
Aidha, ameahidi kupambana na uharibifu wa msitu wa Amazon, ambao ni muhimu katika kuzuia athari mbaya za mabadiliko ya tabia nchi duniani.
Ushindi wa Lula da Silva umetajwa kuwa ni ‘wimbi la waridi’ katika ukanda wa Amerika ya Kusini, baada ya ushindi wa kihistoria wa mirengo ya kushoto nchini Colombia na Chile.
Lula da Silva ni kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi na alizaliwa katika umaskini. Aliongoza mgomo dhidi ya serikali ya kijeshi ya Brazil katika miaka ya 1970.