KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeielekeza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum katika mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Farkwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee mara baada ya ziara ya Kamati ya kukagua miradi ya ujenzi wa Shule ya Msingi Sankwaleto na ule wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Farkwa katika Halmashauri ya Chemba.
Alisema: “Kamati inaagiza CAG (Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) aje kufanya ukaguzi maalum kwenye kituo hiki cha afya cha Farkwa, kwasababu Kamati imeona hakuna thamani ya fedha hapa.”
Alisema, hali ya miundombinu iliyojengwa katika Kituo cha Afya cha Farkwa hauendani na thamani ya fedha ambayo Serikali imekwishatoa katika mradi huo.
Aidha, Kamati pia imeielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kufanya ufatiliaji wa karibu wa miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Chemba ili ikamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange imeitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kuongeza usimamizi wa miradi ya Serikali ili thamani ya fedha ionekane.
“Serikali inaleta fedha kwa ajili ya kuhudumia wananchi na kuna wataalamu wa kutosha kusimamia miradi hiyo, na sera ya Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi hivyo fedha ikitolewa tuisimamie vizuri ili thamani ya fedha ionekane kwenye miradi yetu,” Dkt. Dugange.