WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umewasihi Watanzania kote nchini kuachana na dhana ya kwamba Nishati Safi ya Kupikia ni gharama ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu ametoa rai hiyo Julai 04, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam ndani ya Banda la Maonesho la Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Kumekuwepo na dhana kwamba kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme ni gharama ikilinganishwa na kutumia kuni, dhana hii ni potofu haina ukweli kwani sasa hivi teknolojia imeboreshwa,” alisisitiza Mhandisi Olotu.

Alisema, kwa sasa teknolojia imeboreshwa ikilinganishwa na hapo zamani na alisisitiza kuwa hivi sasa yapo majiko ya umeme ambayo yanatumia umeme kidogo.
Alitoa wito kwa wananchi kutembelea Banda la REA ili kushuhudia teknolojia hizo zilizoboreshwa na kujionea kwa vitendo namna ambavyo majiko hayo yanafanya kazi.
“Wananchi watembelee banda la REA kujionea namna ambavyo chakula kinapikwa kwa kutumia nishati Safi ya Kupikia, ladha haibadiliki na pia muda wa kupika ni mchache ikilinganishwa na chakula kinachopikwa kwa kuni ama mkaa,” alisema.

Akizungumzia kuhusiana na uhamasishaji na uwezeshwaji kwa waendelezaji wa teknojia za Nishati safi ya Kupikia, Mhandisi Olotu alisema lengo ni kuwawezesha Watanzania kutumia nishati safi kuepuka madhara ya afya ikiwemo changamoto kwenye mifumo ya upumuaji sambamba na kulinda mazingira.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya; kwa mwaka mmoja takriban watu 33,000 hupoteza maisha kutokana na matumizi ya nishati isiyo salama na kwamba REA ni miongoni mwa washika dau wa kuhakikisha idadi ya vifo vinavyosababishwa na athari ya moshi ya kuni na mkaa inapungua.
“Tunataka kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa lakini jambo hili linafanyika kwa utaratibu kwani ni ngumu kumbadilisha kila mtu mara moja; inachukua muda na ni hatua kwa baadhi ya maeneo na ndio maana kuna majiko tunasambaza yanayotumia kuni ama mkaa kwa kiwango kidogo,” alisema.

Alisema, kwa kuanzia REA ilianza na mpango wa kugawa majiko ya gesi ya kilo sita ambapo mitungi 3,255 na vichomeo vyake yalitolewa kwa kila Wilaya Tanzania Bara kwa bei ya ruzuku ya 50% na kwamba zoezi hili linaendelea.
“Lengo ni kumhamasisha kila mwananchi kuhama kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa kuja huku kwenye nishati safi ya kupikia na kwa wale ambao tunaona inachukua muda kubadilika tumewaletea teknolojia inayotumia mkaa kidogo tukitaraji taratibu watahama,” alisema.
Vilevile, alibainisha kuwa REA inatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza taasisi zinazolisha Zaidi ya watu mia kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tunatekeleza agizo hili la Mhe. Rais tumeanza kuhamasisha na kuwezesha hizi taasisi kuhama ikiwemo Jeshi la Magereza ambapo maeneo 211 yakiwemo magereza 129, kambi za magereza 47, ofisi za mikoa za Magereza 26, nyumba za watumishi wa Magereza, vyuo, shule na hospitali zinasambaziwa nishati safi mbalimbali za kupikia,” alisema.
Alizitaja nishati zilizosambazwa katika taasisi hizo kuwa ni pamoja na mifumo ya bayogesi, mifumo ya gesi ya mitungi (LPG), mifumo ya gesi asilia, mkaa unaotokana na makaa ya mawe na mashine za kutengenezea mkaa mbadala.
Aidha, alisema wakala vilevile unawajengea uwezo Maafisa wa Magereza wapatao 280 kuhusu suala zima la nishati safi ya kupikia.