MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka viongozi kuzingatia utawala wa sheria na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao.
Kunenge alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu Elimu ya Uraia, Utawala Bora, na Haki za Binadamu kwa viongozi wa Halmashauri za mkoa yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Mafunzo hayo yamewahusisha viongozi wa mkoa, wilaya, na watendaji wa kata kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu misingi ya haki, sheria, na uwajibikaji.
Alisema, uongozi bora unajengwa kwa misingi ya haki na uwajibikaji, hivyo ni jukumu la viongozi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa maslahi ya jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji wa Haki, Lawrence Kabigi, alisema mafunzo hayo yanawasaidia viongozi kuelewa dhana ya utawala bora na haki za binadamu, ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea viongozi uwezo wa kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora kwa maendeleo endelevu ya jamii.