Korea Kaskazini yatangaza rasmi kuwa dola la nyuklia

0

Pyongyang, KOREA KASKAZINI

KOREA Kaskazini imefunga rasmi mjadala juu ya silaha zake za nyuklia, na kutangaza wazi kuwa nchi hiyo ni ya Kinyulia na suala lake la nguvu za Atomika halijadiliki tena.

Kim Jong-un, Kiongozi Mkuu wa Taifa hilo la Mashariki ya Mbali, ametia saini sheria ya kutambuliwa rasmi kwamba ni dola lenye nguvu za kijeshi za nyuklia, muda mfupi baada ya bunge la nchi hiyo kupitisha sheria na kuitangaza rasmi Korea Kaskazini kuwa ni dola lenye nguvu za Atomiki.

Shirika la habari la ‘Pars Today’ limemnukuu Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini hivi karibuni akibainisha kwamba, nchi yake kamwe haitoachana na silaha zake za nyuklia, kwani kumiliki silaha hizo ni udharura wa usalama wa kitaifa.

Wachambuzi wanasema, hatua hizo ni majibu ya wazi na makali kwa ombi la hivi karibuni la serikali ya Korea Kusini, ambayo imeitaka Pyongyang ikabidhi silaha zake za nyuklia na iachane kabisa na siasa zake za kumiliki silaha hizo, ili iweze kufungua miradi yake ya maendeleo na kupata uwekezaji mkubwa wa kiuchumi.

Nalo gazeti la Kimarekani la ‘Washington Post’ Katika makala yake maalumu, limetoa uchambuzi kuhusu Korea mbili likisema kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu ya Ikulu ya Marekani (White House) dhidi ya Korea Kaskazini yameshindwa kabisa.

Gazeti hilo limesisitiza kuwa, Korea Kaskazini imefikia kiwango cha juu ya kujiamini, kiasi kwamba hivi sasa ni dola lenye nguvu za nyuklia na linatumia silaha hizo kuzizuia nchi nyingine hata zisifikirie kuivamia kijeshi nchi hiyo.

“Korea Kaskazini inazihesabu siasa za Marekani kwenye eneo hilo kuwa ni hatari kwa usalama wake” linabainisha.

Ni kwa sababu hiyo, wachambuzi wanasema, ndio maana Pyongyang inalazimika kujiimarisha mno kijeshi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza maradufu kwenye siala hali ikiwemo makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.

Wanasema ingawa Marekani imeiwekea Korea Kaskazini vikwazo vikali mno, lakini vimeshindwa kuipa Washington ilichokuwa inatafuta.

Wanabainisha kwamba, kitendo cha kibeberu cha Marekani cha kupeleka manuwari zake za kivita, katika maji yanayopakana na Korea Kaskazini na China, na kitendo chake cha kuweka mfumo wa makombora ya kisasa huko Korea Kusini, ni miongoni mwa hatua ambazo zinahesabiwa na Pyongyang kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wake.

Wachambuzi wanasisitiza kuwa, hatua ya hivi sasa ya Korea Kaskazini ya kutangaza rasmi kuwa nchi hiyo ni dola lenye nguvu za silaha za atomiki, imefunga milango yote ya kuzungumzia silaha za nyuklia za Pyongyang.

Mara kwa mara Marekani imekuwa ikitaka nguvu za atomiki za Korea Kaskazini ziwekwe mezani kujadiliwa, lakini hivi sasa Pyongyang imetangaza waziwazi kwamba, silaha zake za atomikki si kitu kabisa cha kujadiliwa, na inabidi jamii ya Kimataifa na dunia nzima ikiwemo Marekani itambue kuwa Korea Kaskazini sasa ni dola rasmi la nyuklia.

Mmoja wa wachambuzi hao Hossein Ahan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kwamba, rasi ya Korea imegawika mara mbili.

“Upande mmoja ni ule uliopiga hatua kubwa za kiviwanda yaani Korea Kusini, na upande wa pili ni uliojiimarisha vilivyo kinyuklia yaani Korea Kaskazini,” anabainisha.

Anafafanua kuwa, upande wa kusini wa rasi ya Korea unafanya juhudi za kutumia nguvu zake za utajiri wa kiviwanda, kuushawishi upande wa kaskazini uachane na silaha za nyuklia, ili upate maendeleo ya viwanda.

“Lakini hakuna matumaini hata kidogo kuwa, Korea Kaskazini inaweza kuachana na nguvu zake za nyuklia” anasisitiza.

Amesema, Marekani nayo inaendeleza vitisho vyake kwa Korea Kaskazini suala ambalo si tu linahatarisha usalama wa nchi hiyo, bali linautia hatarini pia usalama wa eneo zima la Asia Mashariki.

Korea Kaskazini nayo haikubakishiwa chaguo lolote jingine isipokuwa kujiimarisha kisilaha, ili kukabiliana na vitisho vya kila kona vinavyoikabili nchi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here