Kongamano la Kitaifa kuhusu uchumi wa bluu kufanyika Septemba

0

OFISI ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) imeandaa kongamano la kitaifa la uchumi wa buluu ili kuwaleta pamoja wadau kujadili dira ya sekta hiyo.

Kongamano hilo litafanyika jijini Dar es Salaam Septemba 10 hadi 11, 2025 na kuwashirikisha washiriki zaidi ya 250 kutoka sekta za uchumi wa buluu za serikali, vyuo vikuu, vijana, wanawake na taasisi zisizo za kiserikali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 22, 2025, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Abdallah Hassan Mitawi alisema, kongamano ni utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Bluu (2024) inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Alisema, Serikali imeweka dhamira ya dhati katika kuhakikisha kuwa rasilimali za bahari, maziwa na mito zinatumika kwa tija ili kuchangia kikamilifu uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Sote tunatambua kuwa uchumi wa buluu unaongeza ajira kwa vijana na kuboresha ustawi wa wananchi bila kuathiri mazingira,” alisema Mitawi.

Aidha, alisema matarajio ya kongamano hilo ni kuziainisha fursa zilizopo katika sekta hiyo na kuonesha kwa namna gani zimebadili maisha ya wananchi na uchumi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa, kongamano hilo litakuwa ni chombo cha utekelezaji wa kisera kinachowezesha mjumuisho wa waau na kutoa mrejesho wa moja kwa moja kwa Serikali kuhusu fursa na mikakati ya kitaifa.

Hivyo, alisema kupitia maazimio yatakayofikiwa, Serikali itaandaa mpango kazi mahsusi wa utekelezaji wa sera, kuvutia uwekezaji, kukuza ajira za vijana na wanawake pamoja na kulinda mazingira ya majini.

Halikadhalika, Naibu Katibu Mkuu Mitawi alisema tayari Idara ya Uchumi wa Bluu imeanzishwa chini Ofsi ya Makamu wa Rais kwa lengo la kuratibu sekta zote zinazohusika na uchumi wa buluu.

Pamoja na hatua hiyo, ili kufanikisha utekelezaji wa Sera hii kikamilifu, kunahitajika ushiriki wa wadau wote katika ngazi zote, ikiwemo sekta binafsi, Asasi za Kiraia na Washirika wa Maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here