Na OR-TAMISEMI
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya maboresho kwenye utoaji wa huduma za Afya msingi kwa kuimarisha miundombinu, vifaa tiba na vitendanishi.
Kuanzia Januari 05, 2023 Kituo cha Afya Gungu kilichopo kwenye Halmashauri ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma kimeanza kutoa huduma ya upasuaji wa wakinamama wanaopata uchungu pingamizi.
Hali hii imeleta furaha na bashasha kwa Jamii ya Gungu kwa kuwa sasa hawatatembea tena umbali mrefu kufuata huduma za upasuaji wa dharura na hii itasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Kituo cha Afya Gungu kilipata fedha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kujenga Jengo la Wagonjwa wa nje, Maabara, Jengo la kufulia, Jengo la Wazazi pamoja na jengo la Upasuaji.
Kituo hiki pia kimepokea vifaa Tiba vilivyowezesha kuanza kutoa huduma ya upasuaji. Majengo hayo yote yamekamilika na kituo hicho kimeanza kutoa huduma rasmi kwa wananchi wa maeneo hato na maeneo ya jirani.