Kinana mgeni rasmi tamasha la kumuombea Rais Samia

0

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye tamasha maalum la kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama alisema tamasha hilo ambalo litawakutanisha jukwaani wasanii mbalimbali wa nyimbo za Injili, linatarajiwa kufanyika Novemba 6, 2022 katika uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza.

“Tamasha hilo linatarajia kuzunguka kwenye mikoa mitano ya Tanzania lengo likiwa kumshukuru Mungu hadi hapa tulipofika,” alisema Msama.

Msama alisema, tamasha hilo ambalo linatarajia kuwa la aina yake, litahusisha waimbaji mbali mbali wa nyimbo za injili kutoka ndani na nje ya nchi akiwemo Rose Mhando, Christina Shusho, Boniface Mwaitege, Eveliny Wanjiru Kutoka Kenya na Joshua Ngoma kutoka Rwanda.

“Nimewataja waimbaji hao wachache tu, lakini wako wengi na wanaendelea kuongezeka kutokana na mazungumzo yetu tunayoendelea kuyafanya baina yetu na wao kuhakikisha tamasha hilo linakuwa la kipekee”, alisisitiza Msama.

Msama aliendelea kusema, “Tunajua Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni mchapakazi na amejitoa kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania, kwa hiyo dhamira ya Tamasha hili ni kufanya maombezi kwa ajili ya kumuomba Mungu aweze kumfanyia wepesi Rais wetu kwenye utekelezaji wa majukumu yake anayoyafanya kwa ajili ya Watanzania.”

Kwa pande wake Mratibu wa Tamasha hilo Emmanuel Mabisa alisema, mpaka sasa baadhi ya mambo yamekamilika na tayari wamezungumza na wachungaji pamoja na Maaskofu mbalimbali ambao wameahidi kushiriki Tamasha hilo la Maombezi kwa ajili ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here