KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi, Kenani Kihongosi, amesema Serikali imetoa Shilingi Bilioni 4.1, huku Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ikichangia Shilingi Milioni 535 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.
Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Mkuranga Boys Technical, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa elimu bora na kuimarisha mafunzo ya ufundi kwa vijana.
Amesema miundombinu inayojengwa inajumuisha madarasa 22, maktaba, majengo ya huduma za afya pamoja na maabara za kisasa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, huku akisisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ili wanafunzi waanze masomo Januari 2027.
Aidha, Kihongosi, amewataka viongozi wa wilaya na mkoa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati, ili wanafunzi waanze kutumia miundombinu hiyo kama ilivyopangwa.
Kwa upande wao, wananchi na viongozi wa eneo hilo wameishukuru serikali kwa uwekezaji huo katika sekta ya elimu, huku wakihimizwa kutunza na kulinda miundombinu ya shule hiyo ili iweze kudumu na kuwanufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo.
Ujenzi wa shule hiyo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuongeza fursa za elimu na kuandaa mazingira yatakayowawezesha vijana kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao ya baadaye.