Kigoma tumieni lami kukuza uchumi – Prof. Mbarawa

0
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila alipokagua moja ya daraja la ndani la watembea kwa miguu katika kijiji cha Makere wilayani Kasulu.

Na Jumbe Abdallah

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa wananchi wa mkoa wa Kigoma kutumia fursa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za lami kufanyakazi kwa bidii na kukuza uchumi.

Alisema, ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Tanganyika, reli ya kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali kuunganisha mkoa huo na dunia, hivyo ni vema wananchi wakatumia fursa hizo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupata maendeleo.

“Takriban KM 400 za lami zinajengwa Kigoma lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha huduma za usafiri na uchukuzi kwa nyanja zote zinaimarika nchini kote ili kuibua fursa zote za uchumi ikiwemo kilimo na biashara”, alisisitiza Prof. Mbarawa.

Muonekano wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.

Akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibondo-Mabamba KM 47.9, Waziri huyo wa Ujenzi amewahakikishia wakazi wote watakaoguswa na mradi huo watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

“Hatutamwonea mtu, kwa vile fidia ni jambo la kisheria wote watakaostahili kulipwa watalipwa”, amesisitiza Prof Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye wakishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9, kati ya Mtendaji mkuu wa TANROADS na Mwakilishi wa Kampuni ya CHICO, mkoani Kigoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema barabara hiyo ya Kibondo-Mabamba yenye urefu wa KM 47.9 inaunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera, Geita na nchi ya Burundi kupitia Gitega hivyo kukamilika kwa ke kwa lami kutachochea biashara katika ukanda wa magharibi.

Alisema, mkandarasi aliyeshinda ujenzi wa barabara hiyo ni kampuni ya CHICO kutoka China na ujenzi wake utatumia miezi 24 ambapo takriban Shilingi Bilioni 63.7 zitatumika.

Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaofanyika Kigoma na kuahidi kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda uliokusudiwa na kutumia fursa ya uwepo wake kupunguza umaskini.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 na kumtaka mkandarasi CHICO anayejenga barabara hiyo kuongeza kasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here