Kazi ya kupeleka umeme kwenye migodi midogo inaendelea – Kapinga

0

📌 Wachimbaji wa chumvi pia wafikiwa

📌 Wananchi Kibiti wampongeza Rais Samia kwa mradi wa umeme wa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.8.

📌 Kituo cha umeme Uhuru wilayani Urambo chakamilika

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi midogo yakiwemo maeneo yanayozalisha chumvi wilayani Bagamoyo.

Kapinga ameyasema hayo Aprili 8, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo, Muharami Shabani Mkenge aliyeuliza ni lini Serikali itapeleka umeme katika eneo la Kitame Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo ili kuwasaidia wazalishaji wa chumvi.

“Hadi kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya maeneo 14 ya migodi midogo imepelekewa umeme ambapo kati ya hayo, maeneo 3 ni ya wachimbaji wa chumvi wanaopatikana katika eneo la Kitame Kata ya Makurunge ambapo jumla ya wachimbaji 34 wanaopatikana katika maeneo hayo wamefikiwa na huduma ya umeme,” alisema Kapinga.

Alisema, kazi ya kupeleka umeme kwa wachimbaji wa chumvi waliosalia itaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.

Aliongeza kuwa, upo mradi mwingine ambao unapeleka umeme kwenye pampu za maji takribani 411 na kwenye maeneo ya kilimo na maeneo ya migodi 605.

Akijibu swali Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe aliyeuliza kuhusu mkakati wa Serikali kupeleka umeme kwenye Kitongoji cha Kitame ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa nishati hiyo, Kapinga alisema katika eneo hilo Serikali inatekeleza miradi ya umeme ya Vitongoji.

Katika hatua nyingine Mpembenwe kwa niaba ya wananchi wa Kibiti amemuomba Judith Kapinga kufikisha pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya umeme ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.8 katika Jimbo la Kibiti.

Kapinga kwa upande wake, alisema Serikali inapokea pongezi za wananchi hao wa Kibiti kwa Rais kutokana na kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya nishati ambayo inasimamiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.

Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Margreth Sitta aliyeuliza ni lini Serikali itakizindua kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Urambo Tabora baada ya kukamilika, Kapinga alisema kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kimekamilika Machi 26, 2025 na wananchi wa Urambo, Kaliua na maeneo jirani wananufaika kupitia kituo hicho cha umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Abubakar Asenga aliyetaka kufahamu ni lini mkakati wa kuvipelekea umeme Vitongoji 15 kwa kila Mbunge utaanza jimbo la Kilombero, Kapinga alisema tayari Serikali imeshampata Mkandarasi wa kupeleka umeme katika Jimbo hilo na ameshaanza kazi katika baadhi ya maeneo na Serikali itaendelea kumsimamia ili aongeze kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here