Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kujengwa Kigoma

0

Na Mathias Canal, Kigoma

SERIKALI kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ina mpango wa kuanzisha kampasi ya MUHAS mkoani Kigoma.

Kampasi hii itajengwa katika Halmashauri ya Ujiji mkoani Kigoma katika eneo la ekari 47.3 ambalo linapakana na eneo litalojengwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi.

Kampasi hii inatarajiwa kuwa na miundombinu itakayotoa mazingira bora ya ufundishaji na kujifunzia, utafiti pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo Oktoba 17, 2022 Wilayani Kasulu wakati wa ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Mkoani Kigoma.

Waziri Mkenda alisema, Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia imetenga kiasi cha Dola za Marekani Milioni 45.5 kwa ajili ya MUHAS. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Dola za Marekani Milioni 15 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika kampasi ya Kigoma.

Kadhalika, Waziri Mkenda amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga ambayo ni moja kati ya Miradi iliyotekelezwa na Wizara ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuboresha Mazingira ya utoaji wa Elimu ya Ualimu nchini.

Prof Mkenda amesema kuwa Ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini (Teachers Education Supports Project – TESP).

Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ulianza Machi 26, 2019 ulikamilika Aprili 22, 2022. Ujenzi umetekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Magharibi chini ya Usimamizi wa Mshauri Elekezi Bureau for Industrial Cooperation (BICO) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, kazi ya utengenezaji na uwekaji wa Samani katika majengo haya inaendelea.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa, Mradi huo umegharimu jumla ya Shillingi za Kitanzania 14,142,554,960.53 ambapo Sh. 12,591,407,901.26 ni kwa ajili ya ujenzi wa majengo na Sh. 1,551,147,059.27 ni kwa ajili ya utengenezaji na uwekaji wa Samani na utakuwa na uwezo wa wa kuchukua wanachuo 800.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here