Jussa ‘aangukia pua’ Chadema

0

Na Mwandishi Wetu


MAKAMU
Mwenyekiti ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu ameangukia pua, baada ya Chadema kukataa ushirika nao katika uchaguzi Mkuu ujao Oktoba, 2025.

Habari za ndani ya Chadema zinabainisha kuwa, ziara ya Makamu Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo na Katibu Mkuu wake Ado Shaibu, kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ilikuwa na lengo la kuomba ushirika na chama hicho.

“Alikuja hapa kujaribu kufanya ushawishi ili baadhi ya majimbo waachiwe kwa kuwa Zanzibar hali kwao sio nzuri kisiasa,” kilisema chanzo chetu kilichopo ndani ya Chadema.

Chanzo hicho kiliendelea kudai kuwa, Jussa kwenye mazungumzo yake alisema, viongozi wao wa Mkoa na Wilaya za Pemba karibu wote wamerudi CCM kutokana na kasi ya maendeleo, Zanzibar hivi sasa.

Kilisema, ili kukinusuru chama chao kiongozi huyo wa ACT aliweka wazi kwamba, itabidi wajikite zaidi Bara, kwani Zanzibar pameshakuwa pagumu hususan Pemba na ana wasiwasi huenda baada ya bunge kuvunjwa, wengi wao watahama chama.

Chanzo hicho kinabainisha kuwa, kero za wananchi ndio ulikuwa mtaji mkubwa wa chama hicho, lakini hivisasa nyingi zimetatuliwa, “hivyo inahitajika nguvu ya ziada kushinda Ubunge Zanzibar achilia mbali Urais.

Hata hivyo, inasemekana Lissu amekataa kushirikiana na chama hicho kwa madai kuwa, msimamo wao haueleweki na ndani ya Chadema hakujatulia, hivyo wanahitaji muda wa kujiweka sawa.

Afrika Leo mara kadhaa lilimpigia simu Lissu, lakini simu yake iliita bila kupokelewa na ile ya Jussa ilikuwa haipatikani na mmoja wa viongozi wa ACT akizungumza kwa sharti la kutokutajwa jina alisema, wapo kwenye vikao vya ndani vya chama kujadili mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho.

“Tupo kwenye kikao nimetoka nje kidogo kuongea na simu yako, kifupi tunajadiliana na wenzetu wa vyama vingine mbadala,” alisema na kukata simu.

Siku za karibuni, Jussa amekuwa akizunguka huku na kule na kufanya mikutano ya hadhara na kubeza jitihada za ujenzi wa shule za kisasa za ghorofa, barabara, hospitali na uwekezaji unaotoa ajira kwa wanzanzibari.

Jussa ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa kuisambararisha CUF Zanzibar, anapambana kuinusuru ACT Wazalendo ambayo hata wabunge wake wanadai ipo ktk wakati mgumu, Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here