Na Mwandishi Wetu, Z’bar
OFISI ya Msajili wa Hazina Zanzibar imeandaa Jukwaa la kwanza la wakuu wa taasisi za uwekezaji wa umma litakalofanyika kwa siku tatu; Mei 11-13, 2025 katika hoteli ya Golden Tulip Airport iliyopo visiwani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumamosi Mei 3, 2025, Msajili wa Hazina Zanzibar Waheed Mohammad Ibrahim Sanya alisema, lengo kuu la Jukwaa hilo ni kuwaunganisha wakuu wa taasisi kutoka taasisi mbalimbali za umma ili kujadili changamoto za pamoja, kubadilishana uzoefu, na kuanzisha mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji wa taasisi zao.

“Kupitia jukwaa hili, wakuu wa taasisi za umma wataweza kuimarisha ushirikiano, kubadilishana maarifa, na kuchochea ubunifu,” alisema huku akitabanaisha kuwa mgeni rasmi atakuwa Hemed Suleiman Abdullah, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Kaulimbiu ya Jukwaa hilo ni “Uongozi Bunifu na Mashirikiano ni Muhimu ili kufikia Maendeleo Endelevu Zanzibar.”