JNHPP kufungua fursa za Utalii na kutoa ajira

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi pamoja na wananchi wa Mikoa ya Pwani na Morogoro kabla ya kuzindua Shughuli ya Kufunga Njia ya Kuchepusha Maji na Kuanza Ujazaji wa Maji kwenye Bwawa la Kuzalisha Umeme (Megawati 2115) la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji Mkoani Pwani Desemba 22, 2022.

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo ameshuhudia shughuli ya kufunga njia, kuchepusha maji na kuanza ujazaji maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Mradi huu ulianza mwaka 2018 baada ya Serikali ya Tanzania kupata Kandarasi ya ujenzi ubia wa kampuni ya Arab Contractors na El-Sewedy kutoka Misri.

Rais Samia alisema, mradi huu ni mojawapo ya miradi mikubwa ya umeme barani Afrika ambapo bwawa hilo litaweza kuweka akiba kubwa ya maji na kuzalisha umeme hata mvua inapopungua.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria Hatua ya Kufunga Njia ya Kuchepusha Maji na Kuanza Ujazaji wa Maji kwenye Bwawa la Kuzalisha Umeme (Megawati 2115) la Julius Nyerere JNHPP kwenye Mto Rufiji Mkoani Pwani Desemba 22, 2022.

Pia, Rais Samia alisema mbali na kusaidia kudhibiti mafuriko ya mara kwa mara ya mto Rufiji bwawa hili litawezesha kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameagiza Wakuu wa Mikoa kuwazuia wananchi wanaochepusha maji katika maeneo mbalimbali hasa katika Bonde la Mto Rufiji na kurejesha maji katika mikondo yake ya asili kwa kuzingatia kanuni za mgawanyo wa maji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme (Megawati 2115) la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji Mkoani Pwani Desemba 22, 2022.

Vile vile, Rais Samia amezitaka Wizara husika kutokutoa vibali vya matumizi ya maji na uwekezaji kwenye shughuli za uzalishaji unaohitaji maji mengi katika maeneo ya juu ya bonde (upstream) na badala yake utumike uwanda wa chini wa mradi.

Kukamilika kwa Mradi wa JNHPP ambao umefikia asilimia 78.68 kutaimarisha na kufungua fursa nyingi za utalii katika eneo la kusini mwa Tanzania hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na hivyo kutoa ajira kwa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwapatia tuzo Marais Wastaafu Ali Hassan Mwinyi pamoja na Dkt. Jakaya Kikwete kutokana na mchango wao katika ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kwenye Mto Rufiji mkoani Pwani Desemba 22, 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here