JKT Queens kuvaana na City Lights FC

0

TIMU ya Wanawake ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya JKT Queens, imepangwa kundi A katika mashindano ya CAF, ukanda wa CECAFA yatakayofanyika katika uwanja wa Azam Complex nchini Tanzania kuanzia Januari 7, 2025.

Timu nyingine zinazounda kundi hilo A ni City Lights Football Academy ya Sudani Kusini, Bahir Dar Kenema Football Club ya Ethiopia na Kenya Academy of Sports kutoka nchini Kenya.

Mashindano hayo yaliyopewa jina la ufupisho la GIFT ( U-17 Girls Integrated Football Tournament) ni mashindano mapya ambayo kwa mara ya kwanza yanafanyika nchini Tanzania na kushirikisha timu nane kutoka Afrika Mashariki (CECAFA).

Timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo, zilizopangwa kundi B ni TDS Girls Academy ya Tanzania, Aigle Noir Football Club ya Burundi, Boni Consilli Girls Vocational Team ya Uganda na Hilaad Football Club kutoka Somalia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na CAF, mashindano hayo ni sehemu ya mkakati wake (CAF) wa kukuza usawa wa kijinsia na kuwezesha kizazi kijacho cha wechezaji wa kike.

Taarifa ya CAF imeendelea kusema kwamba, Shirikisho hilo la Mpira wa Miguu Afrika, limedhamiria kuongeza ushiriki wa wasichana katika soka, katika Bara lote la Afrika, kuhimiza vilabu kuwekeza katika timu za wasichana chini ya umri wa miaka 17 na kutoa njia kwa wasichana kuhama kutoka shule za mpira wa miguu hadi soka la ushindani.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa hatua ya makundi, JKT Queens itaanza kuchanga karata zake Januari 7, 2025, saa 10:00 jioni dhidi ya City Lights FC, 10 Januari 2025, saa 10:00 jioni itapepetana na B.D Kenema FC, kisha itakamilisha mechi zake katika kundi A, 13 Januari 2025, saa 10:00 jioni kwa kucheza na timu ya KAS.

“Matarajio ya timu yetu ya JKT Queens, inayonolewa na mwalimu Esta Chaburuma, ni kufanya vizuri katika mashindano hayo yatakayofikia tamati 18 Januari 2025, na kuwa klabu ya kwanza kukinyakuwa kikombe cha ubingwa.”

Tunatoa rai kwa wapenzi, wadau, mashabiki wetu na Watanzania wote, kutupa ushirikiano na hamasa hasa kwa kufika uwanjani siku za mechi ili kuwashangilia wachezaji wetu, kuwatia nguvu na moyo, kuwawezesha kutembeza Kichapo cha Kizalendo kwa wageni hao kutoka mataifa mengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here