JESHI la Polisi Zanzibar limeeleza kuwa linaendeleza msako maalum katika Mkoa wa Mjini Magharibi kwa lengo la kudhibiti vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani, hususan vinavyofanywa na makundi ya vijana wanaojihusisha na mienendo isiyozingatia maadili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Polisi Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa huo ACP Richard Tadeo Mchomvu alisema, hivi karibuni kumeibuka makundi ya vijana wanaokusanyika ufukweni mwa bahari na kufanya vitendo kinyume na sheria, hali inayotishia maadili na usalama wa jamii.
Katika msako huo unaoendelea, Jeshi hilo limefanikiwa kukamata vyombo vya moto vilivyohusishwa na shughuli hizo, ikiwemo gari aina ya Costa lenye namba za usajili Z 306, lililobeba vijana kwa idadi kubwa waliokuwa wakicheza ngoma barabarani huku wakiwa wamevalia mavazi yasiyozingatia maadili ya Mzanzibari. Vijana waliokamatwa ni wanaume 15 na wanawake 24.
Aidha, magari mengine mawili aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili Z 405 JY na Z 784 LL nayo yalinaswa yakiwa yamebeba spika kubwa za muziki na kushiriki katika misafara hiyo isiyo rasmi.
ACP Mchomvu alisema, vijana waliokamatwa wana umri wa kati ya miaka 19 hadi 29, na akatoa wito kwa wazazi na walezi kusimamia maadili ya watoto wao ili kuwaepusha na majanga yanayoweza kuwapata.
Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani (ZTRA) pamoja na Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu, wataendelea kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa sheria vinadhibitiwa ipasavyo ili Zanzibar iendelee kuwa mahala salama.
Aidha, ametoa onyo kwa wale wote wanaojipanga kwenda fukweni kwa lengo la kujistarehesha kinyume na maadili kuacha mara moja, akibainisha kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Haji Ali Zubeir alisema kuwa watashirikiana na Jeshi la Polisi kukabiliana na waendeshaji wa vyombo vya moto wasio na leseni, huku akieleza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua kali ikiwemo faini au kifungo kulingana na uzito wa makosa yao kwa mujibu wa sheria.