Jeshi la Polisi ni ngao ya jamii katika usalama na maendeleo

0

KATIKA ulimwengu wa sasa, usalama wa raia na mali zao, ni kiini cha maendeleo ya Taifa lolote.

Tanzania ni nchi yenye historia ya amani na mshikamano, hali ambayo inapaswa kuendelea kuimarishwa kwa nguvu zote.

Jeshi la Polisi limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa utulivu na kwamba wahalifu na wanaotaka kuhujumu usalama wao, wanashughulikiwa ipasavyo.

Kamishna wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia Kamisheni ya Operesheni na Mafunzo, CP Awadhi Juma, Machi 6, 2025 akiwa Chuo cha Polisi Kidatu, aliwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia amani na utulivu nchini, hasa kuelekea wakati na baada ya uchaguzi.

Alisisitiza kuwa, hakuna mtu yeyote atakayevuruga usalama wa nchi kwa kisingizio cha siasa au maslahi binafsi.

Kamishna Awadhi alisisitiza kuwa, Polisi hawatakuwa na muhali kwa wale wanaotaka kuvuruga uchaguzi au kuleta taharuki isiyo ya lazima.

“Tumejipanga vizuri kwenye hili, tutashughulika na watu wa hovyo hovyo wanaodhani wanaweza kufanya vinginevyo. Blabla mnazozisikia zisiwanyime usingizi, uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu mkubwa.” anasema.

Kauli hii inaonyesha kuwa wananchi wanapaswa kuwa na imani na Jeshi la Polisi, kwani liko imara kuhakikisha kuwa kila mmoja anaendelea na shughuli zake kwa uhuru bila hofu ya vurugu au uvunjifu wa sheria.

Wanapaswa kujua kwamba, Jeshi hili liko upande wao katika kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kuwa na amani, maendeleo na utulivu wa kudumu kazi ambayo wameifanya kwa miaka mingi, ambapo hivisasa Jeshi hilo limetimiza miaka 60.

Kwa kipindi chote hicho, Jeshi la Polisi limethibitisha kwamba, si adui wa raia wema bali ni kimbilio lao katika nyakati za shida na limeonyesha wazi kwamba, usalama hauletwi na maneno matupu, bali vitendo.

Kwa miaka mingi, Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi kwa karibu na wananchi katika kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani na utulivu. Matukio mbalimbali ya ukatili, uporaji na uhalifu yamekuwa yakishughulikiwa kwa haraka, kuhakikisha wahusika wanakamatwa na sheria inachukua mkondo wake.

Kwa maana hiyo, ili Jeshi hilo liendelee kutimiza wajibu wake, wananchi nao wanapaswa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Hii ni kwa sababu usalama wa nchi ni jukumu la kila mmoja.

Polisi hawawezi kuwa kila mahali kwa wakati mmoja, lakini kwa ushirikiano na wananchi, wahalifu hawatapata nafasi ya kuhatarisha amani ya jamii.

Vile vile, ili kuimarisha ushirikiano huo, ni muhimu pia wananchi wakaelewa kuwa, si kila mtu anayelalamika dhidi ya Jeshi la Polisi ana nia njema.

Wapo wanaolalamika kwa sababu wana maslahi binafsi, wanapenda uvunjifu wa sheria uendelee bila kuzuiliwa. Lakini, kwa wananchi waadilifu, Jeshi la Polisi ni kimbilio la haki na usalama wao.

Kwa upande mwingine, wanaosambaza propaganda dhidi ya Jeshi letu la Polisi, wajue kwamba, wananchi wa sasa wana macho ya kuona mazuri na mabaya. Wanaona jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu na kuhakikisha kuwa Taifa linabaki salama.

Wanaweza pia kunusa pale ambapo kuna harufu ya propaganda zisizo na msingi na kutofautisha ukweli na uzushi. Masikio yao yanasikia taarifa za utekelezaji wa haki, usawa na uwajibikaji ndani ya Jeshi la Polisi.

Wananchi hawawezi kudanganywa, kwani wana akili ya kuchambua na kufanya maamuzi sahihi kuhusu nani ni mlinzi wa kweli wa amani yao.

Wananchi wana mdomo wa kusema wanapofurahia kazi nzuri ya Jeshi la Polisi. Kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, wananchi wanaeleza kuridhika kwao na jinsi Polisi wanavyoshughulikia masuala ya uhalifu na kuimarisha ulinzi wa raia.

Ngozi yao inahisi pale ambapo kuna utulivu na amani, lakini pia wanahisi maumivu wanapoona kuna matukio ya kihalifu yanayoathiri jamii. Hili linazidi kuwafanya waelewe kuwa, Jeshi la Polisi ni nguzo yao katika kuhakikisha hawateswi na wahalifu wanaotaka kuvuruga utulivu wa Taifa.

Namalizia kwa kusisitiza kuwa, Polisi wapo kwa ajili ya kulinda wananchi dhidi ya wahalifu na kuhakikisha kuwa kila mmoja anaweza kuendelea na maisha yake kwa amani na utulivu. Tuwaamini na kuwapa ushirikiano kwa maslahi ya nchi yetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here