‘Jacob Zuma, anapaswa kurudi gerezani’

0

JOHANESBURG, Afrika Kusini

MAHAKAMA Kuu ya Rufaa nchini Afrika Kusini imesema Rais wa zamani wa taifa hilo, Jacob Zuma, anapaswa kurudi gerezani kukamilisha kifungo chake.

Zuma, alihukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani mnamo Juni 2021 kwa kukosa kufika mahakamani, hali iliyozua maandamano makali nchini humo.

Hata hivyo, kiongozi huyo alihudumu kwa miezi miwili pekee gerezani, ambapo baadaye alipewa msamaha wa matibabu.

Msamaha huo ulitolewa na Mkuu wa Idara ya Magereza nchini humo, licha ya ushauri wa kamati ya matibabu ya idara hiyo kwamba Zuma hakuwa ametimiza masharti ya kupewa msamaha huo.

“Mahakama hii imeamua Zuma alipewa msamaha wa matibabu kinyume cha sheria,” ikasema mahakama ya rufaa kwenye uamuzi wake.

“Kisheria, Zuma hajamaliza kutumikia kifungo chake. Lazima arejee katika Kituo cha Kurekebishia Tabia cha Estcourt ili kukimaliza,” ikaeleza mahakama, ikirejelea gereza hilo, lililo kaskazini mashariki wa mji wa Durban.

Zuma, ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioukabili utawala wa ubaguzi wa rangi, alichaguliwa kama rais mnamo 2009.

Hata hivyo, alilazimika kuondoka madarakani 2018 kufuatia madai ya kushiriki katika sakata za ufisadi, ambapo licha ya tuhuma hizo, bado ana umaarufu mkubwa miongoni mwa wafuasi wa chama tawala cha African National Congress (ANC).

Wakati kifungo chake kilipotangazwa, maandamano makali yalizuka katika maeneo tofauti nchini humo, hali iliyosababisha vifo vya watu 350. Maduka kadhaa pia yaliporwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here