Na Munir Shemweta, Mwanza
MBUNGE wa Jimbo la Ilemela ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo la hilo.
Dkt. Mabula alitoa shukran hizo jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM wilaya ya Ilemela kwa kipindi cha mwaka 2020-2022 kwenye Mkutano Maalum wa Wajumbe wa CCM wilayani humo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, utekelezaji huo wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ni ya kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba 2022 ambapo taarifa ya mapokezi ya fedha imegusa kipindi cha miaka miwili ya utendaji wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika utoaji wa pesaza miradi ya maendeleo katika jimbo la Ilemela.
‘’Hakika tunajivunia kuwa na rais mwenye maono mwenye kujali ustawi wa watu anaowaongoza kwa kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia watanzania wote kwa wakati,’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Ilemela, katika kipindi cha miaka miwili halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hadi kufikia Machi 2023 imepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 46.089 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ameitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa ufanisi katika jimbo lake kuwa ni pamoja na sekta ya ardhi, afya, elimu, maji, miundommbinu, uvuvi, pamoja na masoko na biashara.
Akielezea kuhusiana na sekta ya ardhi anayoisimamia, Dkt Mabula alisema katika kutekeleza azma ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kupitia fedha za mkopo zilizotolewa na Rais Samia, manispaa ya Ilemela imekuwa mnufaika mkubwa wa fedha hizo kati ya halmashauri 58 zilizonufaika na mkopo huo nchini.
Amebainisha kuwa, kupitia mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi manispaa ya Ilemela imepima viwanja katika maeneo ya Buswelu, Nyafla, Sangabuye,Igalagala na ilekelo ambapo mradi umekamilika na viwanja 3,254 vimepimwa kwenye ekari 900 zilizopimwa na kugharimu kiasi cha Shilingi 3,589,774,000 kutoka serikali kuu.
‘’Mpaka sasa manispaa imefanikiwa kuuza viwanja katika mradi husika kwa asilimia 70% na kufanikiwa kurejesha mkopo kwa asilimia 100%’’ alisema Dkt. Mabula.
Kwa upande wake Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa aliyekuwa mgeni maalum kwenye mkutano huo Sophia Mjema alimpongeza mbunge wa jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula kwa kufanikisha utekelezaji ilani ya chama hicho katika jimbo lake.
Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi Innocent Bashungwa, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Naibu Waziri Kilimo Anthony Mavunde na Naibu Waziri Malisili na Utalii Mary Masanja, Mjema aliwataka viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya kuhakikisha wanawaeleza wananchi yote yaliyoahidiwa na kutekelezwa kupitia ilani ya CCM.
“Tunapoenda kutekeleza haya ni lazima tuwaeleze wananchi tuliyoahidi kwa kutoa taarifa tulipotoka, tulipo na tunapoelekea na hapo ndiyo tunahakikisha ilani inatekelezwa ipasavyo,” alisema Sophia Mjema.
Katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbali na mambo mengine Halmashauri ya Ilemela imepata mafanikio mbalimbali kama vile kufungua shule 5 mpya za sekondari, kukamilisha na kufungua zahanati 3, kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya kayenze pamoja na majengo muhimu ya hospitali ya wilaya na huduma za wagonjwa wan je zinazotolewa.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Ilemela Dkt. Mabula kupitia taasisi yake ya Angeline Foundation alitoa pikipiki 16 kwa watendaji wa jimbo lake zilizokabidhiwa na Katibu wa Itikadi na Uwenezi wa Chama cha Mapinduzi Sophia Mjema ambapo pia mbunge huyo wa Ilemela atatoa basi kwa ajili ya kusaidia shughuli za halmashauri ya wilaya ya Ilemela.