ICTC kuwakutanisha wataalamu 300 jijini Arusha

0
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga (kushoto), akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.

TUME ya TEHAMA (ICTC) imeandaa Kongamano kubwa la usalama wa mitandao litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 4, jijini Arusha na kuwakutanisha wataalamu zaidi ya 300.

Katika juhudi za kuunga mkono uwezeshaji wanawake katika eneo hilo, Tume hiyo imetangaza kufadhili wanawake 100 waweze kushiriki katika Kongamano hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati akitangaza kuhusu kongamano hilo mbele ya waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam alisema, huo ni sehemu ya mikakati ya ICTC na Serikali kwa ujumla kuimarisha usalama mtandaoni ili uchumi wa Tanzania uweze kupaa na kuwa endelevu.

“Lengo la mkutano huo ni kuimarisha usalama wa mtandao wa Tanzania kupitia ushirikiano, ubadilishanaji wa maarifa, na uvumbuzi…Nchi yetu kwa sasa ipo katika mikakati ya haraka sana ya kufanya mapinduzi ya Kidigitali ili tuweze kupata faida ya mambo mengi ambayo yapo duniani na yanaletwa na teknolojia hii ya TEHAMA,” alisema Dkt. Mwasaga.

“Duniani ili uwekezaji uweze kukua, usalama mtandaoni ni suala muhimu sana kujadiliwa,” alisisitiza na kubainisha kuwa, kongamano hili litashirikisha zaidi ya wataalamu 300, kati yao 100 kutoka katika Mataifa mbalimbali yenye kujikita katika TEHAMA.

Alisema, pamoja na kuwa Tanzania ni ya pili kwa usalama mtandaoni Barani Afrika, ikitanguliwa na Mauritius ni lazima kuendelea kuhakikisha kwamba usalama unaendelea kutokana na kuibuka kwa teknolojia mpya zinazofungamanishwa na teknolojia ya TEHAMA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here