Iddy Mkwama
HIVISASA, Muungano wa nchi mbili huru; Tanganyika na Zanzibar ndio ambao unatajwa kuwa imara na uliodumu kwa muda mrefu zaidi Barani Afrika, huku ukitajwa kuwa wa kupigiwa mfano na nchi nyingi ambazo zilijaribu kuungana, lakini baadae wakashindwa kuelewana, wakasambaratika.
Huu ni Muungano ambao hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwake ilisainiwa Aprili 22, 1964 kati ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kisha yakafuatiwa matukio mbalimbali ya Muungano ambayo yalihitimishwa Aprili 26, 1964.
Ni Muungano ambao umedumu kutokana na mizizi yake ambayo imechangiwa na historia ya uhusiano wa udugu wa damu, harakati za pamoja na ushirikiano wa vyama vya ukombozi vya Tanganyika na Zanzibar katika kupigania uhuru.
Dkt. Abdallah Mkumbukwa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), wakati akitoa mada kuhusu upekee wa Muungano huu, kwenye semina kwa wahariri wa vyombo vya habari, iliyofanyika Disemba 23, 2025, jijini Dar es Salaam chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauwezi kufananishwa na wowote ule ambao upo au umewahi kuwepo.

Anasema, zipo nchi nyingi ambazo zilijaribu kuungana, lakini wameshindwa kudumu kwenye umoja kama ilivyo kwa Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 61 na bado unaendelea kuimarika, huku changamoto mbalimbali zikiendelea kutatuliwa.
Dkt. Mkumbukwa anasema, kudumu kwa Muungano huo, ni moja ya mambo yanayoufanya kuwa wa kipekee, ikizingatiwa nchi nyingi zilijaribu kuungana, lakini miaka michache baadae zikashindwa kuendelea kuwa pamoja.
Akitaja baadhi ya nchi ambazo ziliwahi kuungana, Dkt, Mkumbukwa anasema, mwaka 1952, Ethiopia na Eritrea waliungana, ambapo Muungano wao ulidumu kwa miaka kumi kisha ukavunjika.
Inaelezwa, chanzo cha kuvunjika kwa Muungano huo zipo nyingi, lakini kubwa ni malalamiko ya upande mmoja wa Eritrea ambayo ilikuwa nchi ndogo, ikilalamika kuna mambo hayaendi sawa kwa mujibu wa makubaliano yao.
Mbali na Muungano huo, kulikuwa na ule uliohusisha Ghana na Guinea mwaka 1958, ambao ulizaa Muungano mwingine katika ya Ghana, Guinea na Mali, nao haukukaa muda mrefu, hivisasa kila nchi ipo peke yake.
Kulikuwa na Muungano kati ya Misri na Syria ambao ulianzishwa mwaka 1958, ukadumu hadi mwaka 1971, ingawa inaelezwa ulikufa miaka miwili baada ya kuanzishwa yaani mwaka 1961, ingawa jina la Muungano liliendelea kubaki, hadi ulipokufa rasmi.

Vile vile, kulikuwa na Shirikisho la SeneGambia, nalo lilikaa kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1989. Hili liliunganisha baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama, Uchumi, sarafu moja, sera ya mambo ya nje, bunge, ofisi ya Rais na Mahakama.
“Shirikisho hili lilivunjika kwasababu ya malalamiko kwamba upande mmoja hautendewi haki na upande mwingine, kwahiyo Muungano ukavunjika, ni tofauti na Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar ambao una miaka 61, mingine yote ilikufa,” anasema Dkt. Mkumbukwa.
Pia, anasema kulikuwa na Muungano wa Rwanda na Burundi ambao kwa miaka kadhaa waliishi pamoja, hata makabila makubwa ya Wahutu na Watusi yapo pande zote mbili, lakini mpaka sasa hawaelewani.
Kuna nchi za Afrika Kusini na Namibia, hawa wana historia inayofanana, Kijiografia, wapo karibu, lakini mpaka sasa ni nchi mbili tofauti, “kwa hiyo ukiangalia kuna nchi Kijiografia zinakaribiana sana, ni tofauti na Tanzania Bara na Zanzibar, tunatenganishwa na Bahari, ni tofauti na Rwanda na Burundi, hawatenganishwi na kitu chochote, ni mipaka tu iliyochorwa. Afrika Kusini hawatenganishwi na kitu chochote, wanashirikiana kwenye mipaka yao, lakini kila nchi ipo peke yake.”

Mfano mwingine alioutoa Dkt. Mkumbukwa ni nchi ya Sudan, ambayo ilikuwa moja, lakini hivisasa kuna Sudan na Sudan Kusini ambao kwa muda mrefu sasa hawana maelewano. “Pia, kulikuwa na Shirikisho la Mali na Senegal. Halikukaa muda mrefu, likasambaratika.”
Aidha, anasema mwaka 1967 ilianzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikihusisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ikavunjika mwaka 1977, “unaweza kuona ni mfano mmoja wapo, nchi zinaungana vizuri, lakini yanakosekana maelewano, zinasambaratika. Jumuiya hii ilianza tena miaka ya tisini, kisha ikahuhishwa miaka ya 2000 na mpaka sasa tunakwenda vizuri.”
Mbali na kudumu kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dkt. Mkumbuka anasema, upekee mwingine wa Muungano huo ni muundo wake ambao haupo popote pale duniani.
“Sio Muungano Jumuishi wala Shirikisho. Ni muundo wa kipekee. Tuna Muungano wa nchi mbili huru, lakini tuna Serikali mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa upande wa uwakilishi wa wananchi, tuna bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, na baraza la wawakilishi Zanzibar,” anasema.
Aliongeza: “Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na mambo mengine, linatunga sheria zinazotumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza la wawakilishi linatunga sheria ambazo zinatumika Zanzibar pekee, lakini sheria ambazo zinatungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zitakwenda kutumika Zanzibar, ni lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupata baraka na zitumike Zanzibar.”
Upekee mwingine kwa mujibu wa Mhadhiri huyo ni kwamba, Muungano huu ulianzishwa kwa amani na makubaliano, haukuanzishwa kwa nguvu. Ni tofauti na iliyowahi kuwepo duniani kote ambayo ilitokana na vita, shinikizo la kijeshi, kikoloni, au utawala wa Kifalme.

“Muungano wetu ulitokana na historia ya udugu, mahusiano ya muda mrefu wa watu wa pande zote mbili za Muungano, ulitokana na makubaliano ya hiari ya viongozi wetu wakati ule. Naweza kusema Muungano ulikuwepo kabla, lakini baadae ulifanywa kuwa rasmi na kuijulisha dunia kwamba sasa tumeungana,” anasema.
Akifafanua zaidi anasema, Tanganyika na Zanzibar zilikuwa ni nchi ambazo tayari zilikuwa zimeungana, kwani kulikuwa na mambo yanafanyika kwa kushirikiana ikiwemo kupigania uhuru na ukombozi wa nchi hizi mbili, “kulikuwa na ushirikiano mkubwa kama nchi moja, lakini zilikuwa nchi mbili tofauti, mwaka 1964 Muungano ukawa rasmi.”
Jambo jingine la kipekee, ni Muungano ambao unaunganisha nchi moja ya Bara na nyingine ambayo ni Kisiwa, ambapo anasema ni nchi chache duniani ambazo zinaunganisha Bara na Kisiwa kwa mtindo kama huu kwani, mara nyingi visiwa vinataka uhuru zaidi, ukilinganisha na nchi nyingine za bara.
Alitolea mfano wa visiwa vya Comoro ambavyo vipo vinne. Lakini vilivyobaki kwenye Muungano ni vitatu, kimoja Mayotte kilikataa kujitoa na waliendelea kubaki chini ya Ufaransa, “vitatu vimebaki kuwa sehemu ya Comoro. Indonesia, ni Muunganiko wa visiwa vingi, ila kuna eneo moja Aceh, ambalo lipo Kaskazini, mara kwa mara wanataka kuwa huru zaidi na kuwa na madaraka zaidi kuliko wengine katika nchi hiyo.”

Pia, anasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umehifadhi utambulisho wa pande zote. Kwamba, Zanzibar imebaki na jina lake, rais wake, serikali yake, bendera, wimbo wa Taifa, sheria zake za ndani, Katiba yake, pia kuna utambulisho wa tamaduni zake.
“Ni nadra sana kuwa na nchi mbili zilizoungana zikabaki na utambulisho wake bila kuathiri muundo na umoja wa Muungano, haya yanafanyika Tanzania na Muungano unaendelea,” anasisitiza.
Dkt. Mkumbukwa pia anasema, Muungano huu ni chachu ya amani na utulivu na maendeleo, kwani ndio umewezesha uwepo wa amani na utulivu wa kisiasa na diplomasia imara Afrika Mashariki, “kwahiyo tumeendelea kusimama kama dola na kushiriki Kimataifa kama dola imara wakati majirani wengi wamepitia kwenye migogoro. Tanzania imeendelea kubaki kuwa na amani ikichangiwa na Muungano wetu ambao ni Madhubuti na hilo limechangia kudumu kwa Muungano huu.
Anasema, upekee mwingine wa Muungano huu ni kuwa kichocheo cha ujenzi imara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani umeifanya Tanzania kuwa nchi yenye uimara wa kisiasa, ni alama au ishara katika ushirikiano wa Kikanda.
“Tanzania imekuwa alama na uimara wa utulivu wa kisiasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, kwa muktadha huu, utaona nchi nyingi zina fursa ya kujifunza mengi hasa katika kushughulikia hoja mbalimbali zinazojitokeza katika Muungano kabla hazijakua na kuhatarisha uimara wa Muungano.”
Anasema, kuna utaratibu mzuri umewekwa ambapo ikitokea hoja yoyote kuhusu mambo yanayoendelea kwenye Muungano, imeundwa Kamati Maalumu inayoshughulikia hoja hiyo. Ni kamati inayohusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinnduzi Zanzibar.
“Kama vyombo vya habari, tuna wajibu na kazi muhimu wa kuhakikisha upekee huu wa Muungano unafahamika, unathaminiwa, unalindwa na unaenziwa kwa maslahi yetu kama Taifa vizazi vijavyo na karne na karne,” anasisitiza Dkt. Abdallah Mkumbukwa.