Hoja za Tundu Lissu za ‘No Reform, No Election’ ni dhaifu -Mbeto

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimetaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuachana na hoja dhaifu ya ‘No Reform No Election’ na badala yake wakitengeneze chama chao kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu l.

Akizungumza na wanahabari leo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis alisema, Tume ya Uchaguzi ipo kwa mujibu wa kifungu cha pili cha katiba ya mwaka 2024, ambapo kifungu namba 27 kinaeleza kuwa tume itakuwepo kwa miaka mitano.

“Wao wasubiri tume itangazwe na sio kushinikiza na hata suala la uchaguzi kusogezwa mbele halina nafasi kwani itakuwa ni uvunjifu wa katiba,” alisema.

Mbeto alibainisha kuwa, katiba inabainisha kuwa uchaguzi utaahirishwa iwapo tu kuna kifo cha mmoja wa wagombea na sio suala la kushinikiza.

Alisema, Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu anapoilalamikia tume anasahau 2015 wakiwa na UKAWA walishinda majimbo karibu yote katika miji mikubwa ikiwa na mgombea wao wa Urais alifikisha hadi asilimia 40 ya kura zilizopigwa.

“Wakati huo ilikuwa tume gani? Waache kelele” alisema na kuongeza, hata anapolalamikia Uchaguzi Mkuu wa 2020 hana hoja kwani sheria za uchaguzi na katiba vipo wazi.

Alisema, kama uchaguzi huo kulikuwa na udhaifu wa kiutendaji hilo ni suala jingine, kwani sheria na katiba vipo wazi na CCM wanaheshimu katiba.

Mwenezi huyo alisema, ndio maana chama hicho kikafanya mageuzi katika sheria zake za kuwapata wagombea lengo ni kupanua zaidi wigo wa demokrasia.

Mbeto amewataka viongozi wa Chadema kujitafakari na watambue kuwa, CCM inaposema uchaguzi upo ni kwa mujibu wa katiba na sio vingine.

Siku za karibuni Tundu Lissu amekuwa akisema kuwa, iwapo hakutakuwa na mabadiliko, hakutakuwa na uchaguzi, huku akisisitiza watahamasisha umma kuzuia uchaguzi huo.

Lissu anaenda mbali zaidi kwa kushinikiza iwepo Tume Huru ya uchaguzi na ya sasa ivunjwe ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni kinyume cha katiba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here