Na Mwandishi Wetu
MENEJA Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) James Mlowe, amesema moja ya mbinu wanazotumia matapeli wanaowaibia fedha wastaafu, ni kuchukua taarifa zao muhimu kupitia kwa maafisa waajiri na kisha wanazitumia kufanya uhalifu huo.
Mlowe alisema hayo, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi baina ya Mfuko huo na Chama Cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC), ambapo aliwataka wastaafu wa mfuko huo kuwa makini na matapeli hao pindi wanapokuwa kwenye mchakato wa kufuatilia mafao yao na wanapopata fedha zao.
“Teknolojia pamoja na faida zake, lakini kuna watu wanaitumia vibaya kuwatapeli wazee wetu ambao wamestaafu baada ya kufanya kazi kwa miaka mingi, wanatafuta taarifa zao muhimu, kisha wanawapigia simu na mtu akiwa na taarifa zako ni lazima utampa ushirikiano,” alisema Mlowe.
Aliendelea kusema, walifanikiwa kuwakamata baadhi ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na utapeli wa mitandao, na baada ya kuwabana walieleza mbinu wanazotumia kupata taarifa hizo, ambapo wamekuwa wakiwapigia maafisa wanaohusika na ajira za watumishi hao na kujitambulisha wanatoka TAMISEMI na kuomba taarifa za wanaotarajia kustaafu.
“Wanasema huwa wanapiga simu kwa waajiri mfano wanapiga kwenye Halmashauri ambako inajulikana watumishi wengi wameajiriwa huko, wanaomba taarifa za watu wanaokaribia kustaafu ikiwemo majina yao kamili, namba za simu na taarifa nyingine za ajira, kisha wanawapigia na kuwatapeli,” alisema Mlowe.
Alisema, mara nyingi wastaafu hao wamekuwa wakiambiwa watume kiasi cha fedha ili kulipia gharama kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya taratibu za malipo yao, na wanapewa namba za simu ili wafanye malipo hayo, ambapo wastaafu wengi wamekuwa wakituma na kutapeliwa “wanapaswa kujua kwamba, hakuna malipo ya Serikali yanayofanywa kupitia simu ya mkononi, malipo yote yanafanywa kupitia Control number.”
Aidha, alisema wengine wamekuwa wakitapeliwa fedha zao ambazo wamehifadhi kwenye akaunti, jambo ambalo linasababisha wastaafu wengi kuwa kwenye wakati mgumu “inauma sana mtu kufanya kazi kwa miaka mingi, kalipwa mafao yake halafu anatapeliwa fedha zake zote, tuwasaidie wazee wetu ili wasiendelee kutapeliwa, wakielewa suala hilo, huu utapeli utakwisha.”
Mbali na hilo, Mlowe alisema kuna wakati baadhi ya matapeli walikuwa wanakwenda kwenye ofisi za PSSSF na kuangalia namba za wastaafu wanaojindikisha kwenye daftari la wageni wanaokwenda kwenye ofisi za Mfuko huo na kisha wanawapigia na kuwatapeli.
“Wakishapata namba za wastaafu hao, wanawapigia na kuwaambia wanaweza kuwasaidia ili wapate mafao yao kwa haraka, na hatimaye wanawatapeli, kwa hiyo natoa wito kwa wastaafu kuwa makini na wasikubali kutoa taarifa zao wa watu wasiowajua, familia nazo ziwasaidie kuwapa elimu wazee wetu hawa ili wasitapeliwe,” alisisitiza.
Aidha, Mlowe alitoa wito kwa waandishi wa habari kusaidia kutoa elimu kwa wastaafu kutomtumia mtu yeyote taarifa zake za kustaafu: “Mstaafu anapopokea barua ya kustaafu anatakiwa kuanza hatua ya kufuatilia mafao yake, hivyo anatakiwa kwenda hatua inayofuata ya kuchukua fomu ya PSSSF na kujaza ili kupeleka kwa mwajili wake na sio kufanya mawasiliano na mfanyakazi yeyote.”
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mbali na jitihada zinazofanywa na PSSSF ili kuhakikisha suala la utapeli kwa wastaafu linakomeshwa, Serikali nayo inapambana kukabiliana na tatizo hilo, ambapo wameweka mikakati mbalimbali na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, aliwahi kuonya wale wote waliojiandaa kufanya utapeli huo.
Waziri Mhagama alitoa onyo hilo Agosti 4, 2021, wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022, iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la Golden Jubilee Towers, jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kuanza utaratibu huu wa mafunzo, Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wetu, Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia ya kulinda wastaafu, jambo hili la kuwatapeli wastaafu tunataka kulikomesha mara moja na tunaomba vyombo vinavyohusika na vile ambavyo vipo hapa leo ninapofunga mafunzo haya na wao waanze mkakati wa kubaini matapeli wote ndani ya Serikali na nje ya Serikali wanaojihusisha kuangamiza maisha ya wastaafu wetu.” alisisitiza.
Waziri Jenista aliwaasa wastaafu hao watarajiwa kuwa makini kwa kufuata vyanzo sahihi vya utoaji taarifa za Mfuko ili kujiepusha na taarifa za watu wenye nia mbaya.