Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amekanusha taarifa zilizozagaa mtandaoni kuwa Serikali imeingia mkataba na kampuni mojawapo ya Saudi Arabia, kuwekeza eneo maalum la uchumi la Bagamoyo ikiwemo Bandari.
Prof. Kitila ametoa ufafanuzi huo leo, Ijumaa 14 Februari katika Bunge la 12, Mkutano wa 18, Kikao cha kumi na nne, baada ya Naibu Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu kumtaka atoe tamko kuhusiana na habari hizo zinazosambaa mitandaoni kuhusiana na uwekezaji Bandari ya Bagamoyo.
“Mheshimiwa Waziri kabla ya yote toa tamko kuhusiana na habari zilizosagaa mtandaoni kuhusiana na eneo maalum la uchumi ikiwemo Bandari ya Bagamoyo,” alisema Naibu Spika Zungu.
Prof. Kitila alianza kwa kueleza vipengere sita ambavyo ni lazima vifuatwe ili kukamilisha uwekezaji na kubainisha kuwa taarifa zinazosambazwa hazina ukweli wowote.
“Hatuna makubaliano wala mkataba wa eneo hilo maalum la kiuchumi na kampuni yoyote na taarifa kuwa tumeingia mkataba na kampuni ya Saud Arabia eneo la Uchumi la Bagamoyo hayana ukweli,” alisema.