Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia kwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba imetoa miezi miwili kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vijiji inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumaliza kazi walizopewa vinginevyo wataenguliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka wakandarasi ambao wanasuasua katika utekelezaji wa miradi yao kwa mujibu wa mikataba waliyosaini, wahakikishe wanatumia muda huo kujiweka sawa “Kama ulikuwa umesuasua, uko nafasi za chini au ya mwisho, tumia muda huo wa miezi miwili kupanda ili ufike kwenye nafasi inayotakiwa.”
Waziri Makamba alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo, kwenye kikao kilichofanyika JNICC, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wataalamu kutoka REA, TANESCO na Wizarani.
“Serikali haturidhishwi na kasi na mwenendo wa upelekaji wa umeme vijijini, tumetimiza wajibu wetu, lakini bado kasi ni ile ile,” alisema Makamba na kutolea mfano jinsi walivyowawezesha wakandarasi kuendelea na kazi zao wakati bei ya vifaa zikiwemo waya na Transfoma zilipopanda.
Alisema, kufuatilia mfumuko huo wa bei, utekelezaji wa miradi ya REA ulisimama baada ya wakandarasi kushindwa kumudu kununua vifaa hivyo, lakini walikaa nao na kuwasikiliza na kuwaongezea fedha ili wanunue vifaa na waendelee na kazi, lakini bado wapo ambao wanasuasua.
Waziri Makamba alisema, Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo haiwezi kukubali kuona Wananchi wakiendelea kulalamika kutokana na kucheleweshwa kwa miradi husika.
Aidha, Waziri Makamba alisisitiza kuwa, kwa wale ambao wana utekelezaji duni zaidi na hawabadiliki, Serikali itawachukulia hatua za Kimkataba, lakini pia itawashtaki kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Contractors Registration Board) ili waondolewe katika orodha ya Wakandarasi wa Tanzania.
“Kuna malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wabunge, hatuwezi kuwekeza fedha nyingi halafu unatelekeza ‘site’ na kusababisha malalamiko kila kona, tutawaengua, nitasimamia mwenyewe ili kujua kama barua zimefika (Bodi ya Usajili wa Wahandisi) na hatua zimechukuliwa,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy amewakaribisha Wakandarasi wenye kuhitaji mazungumzo au msaada wowote kutoka REA, huku akiahidi kuendelea na utaratibu wao wa kushughulikia kwa haraka malipo ya wakandarasi pale wanapowasilisha madai yao.
“Sisi REA tumeshakubaliana na kuweka mikakati ya dhati kwamba, hatutachelewesha malipo kwa Wakandarasi ila wahakikishe wamekamilisha kazi na wana nyaraka zote, kwani tunatambua umuhimu wa miradi hiyo kwa wananchi,” alisema Mhandisi Saidy.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya NAMIS Corporate, Mhandisi Thomas Uiso, akizungumza kwa niaba ya Wakandarasi wenzake alisema, wamepokea maelekezo ya Waziri Makamba na kuahidi kuyafanyia kazi.
“Mheshimiwa Waziri tumepata maelekezo, tutayafanyia kazi kwasababu tunataka tuendelee kuwepo, tunaamini tutafanya mabadiliko makubwa ndani ya muda tuliopewa,” alisema Mhandisi Thomas Uiso.