WAZIRI Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha mradi wa Bwawa la Maji Kidunda hausimami na unakamilika kwa wakati ili uanze kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Januari 02, 2026) wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa mradi huo unaakisi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha anakabiliana na changamoto ya upungufu wa maji hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
“Kiongozi wetu anaona mbali; aliamua kuutekeleza mradi huu katika kipindi ambacho kulikuwa na utekelezaji wa miradi mingine mikubwa na ya kimkakati iliyotumia fedha nyingi. Serikali inachukua hatua ili kukabiliana na changamoto za Watanzania.”
Wakati huohuo, Dkt. Mwingulu ameiagiza Wizara ya Maji wahakikishe wanaandaa jedwali litakalomsaidia mkandarasi katika utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo utakaogharimu Shilingi Bilioni 366 kutasaidia kuzalisha takribani megawati 20 za umeme.
Amesema mbali na kutoa huduma ya maji, mradi huo utawezesha ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilomita 72.
Ameongeza kuwa mradi huo utasaidia kuhifadhi lita Bilioni 190 za maji zitakasaidia matumizi ya nyumbani hasa kipindi cha ukame wakati kina cha mto Ruvu kinapopungua.
Naye, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema mradi huo utasaidia katika sekta ya kilimo kwani eneo kubwa linalozunguka bwawa hilo ni zuri kwa ajili ya shughuli za kilimo hivyo wizara itawezesha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo hayo.