Dkt. Mwinyi: Tutaendelea kuwawezesha wavuvi, wachuuzi na wajasiriamali

0

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha wavuvi, wachuuzi na wajasiriamali ili kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa wananchi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Septemba 30, 2025, alipokutana na wavuvi, wachuuzi wa samaki na wajasiriamali wa Diko na Soko la Samaki la Malindi, wakati akiendelea na kampeni zake na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema Serikali itaandaa utaratibu mzuri wa usimamizi wa masoko ili kumaliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wajasiriamali katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaongeza fedha za mikopo maradufu, kutoka Shilingi Bilioni 96 zilizotolewa awali, na kusisitiza kuwa wale ambao hawakupata katika awamu ya kwanza watapatiwa nafasi katika awamu inayofuata.

Vilevile, ameahidi kuendeleza ujenzi wa madiko na masoko ya samaki pamoja na maeneo ya wajasiriamali Unguja na Pemba, sambamba na kuwapatia wavuvi boti na vitendea kazi vya kisasa vitakavyowawezesha kufanya uvuvi wa bahari kuu kwa ufanisi zaidi.

Halikadhalika, Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa makundi hayo na wananchi kwa ujumla kumchagua tena ili aendelee kutekeleza ahadi zake na kuleta maendeleo zaidi kwa Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here