Dkt. Mwinyi aahidi mradi mkubwa wa maji Kaskazini Unguja

0

MGOMBEA wa Kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itajenga mradi mkubwa wa maji ili kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wanapata maji ya kutosha na ya uhakika.

Dkt. Mwinyi alitoa ahadi hiyo Septemba 22, 2025, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Uwanja Shangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Ameeleza kuwa Serikali imeingia makubaliano na Kampuni ya NEC kutoka Oman kwa ajili ya kufanikisha mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani milioni 26, hatua itakayopunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa barabara zote kuu na za vijijini zitajengwa kwa kiwango cha lami, ili kuimarisha usafiri na kuongeza fursa za maendeleo vijijini.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Mangapwani pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kigunda, Nungwi, miradi mikubwa ambayo ikikamilika itabadilisha sura ya Mkoa wa Kaskazini Unguja na kuufanya ufanane na mikoa mingine yenye maendeleo makubwa.

Kuhusu uchumi wa buluu, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaimarisha uwekezaji katika sekta ya uvuvi na mwani kwa kuwapatia wavuvi boti za kisasa pamoja na kujenga kiwanda cha kusarifu mazao ya baharini, ili kuongeza thamani ya mazao na kukuza kipato cha wananchi.

Vilevile, ameeleza kuwa Serikali itaimarisha kilimo cha mpunga kwa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya Kibokwa na Cheju, ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa wananchi waendelee kukiamini na kukichagua Chama Cha Mapinduzi, kwani ndicho chama pekee kinachotekeleza kwa vitendo ahadi zake za maendeleo kila mara baada ya kampeni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here