MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji maji ili kuongeza uzalishaji wa kilimo cha mpunga.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 11, 2025, alipokutana na wakulima wa mwani, mpunga na wavuvi wa Chwaka, Cheju na Marumbi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo wa Marumbi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuwasaidia wakulima kwa kuwapatia vifaa bora vya kisasa ikiwemo powertiller, matrekta na mashine za uvunaji (harvester), sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea, viatilifu na mbegu bora kwa wakati muafaka ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mpunga.
Amesema kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikiagiza mchele kutoka Tanzania Bara na nje ya nchi, hivyo Serikali imejipanga kuwawezesha wakulima kuzalisha mpunga zaidi ili kujitosheleza kwa chakula na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa hiyo.
Vilevile, Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar kwa sasa inaongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa mwani, na Serikali inaendelea kuimarisha sekta hiyo kwa kuwajengea uwezo wakulima ili kuongeza uzalishaji.
Amefafanua kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua mwani unaozalishwa nchini, sambamba na kuongeza bei kutoka Shilingi 700 hadi 1,000 kwa kilo, hatua itakayowaongezea kipato wakulima.
Amesema pia Serikali inalenga kujenga viwanda vya kusarifu mwani ili kuongeza thamani ya zao hilo, na kuwapa wakulima fursa ya kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani badala ya kuuza malighafi pekee.
Dkt. Mwinyi amewahakikishia wakulima na wavuvi kuwa Serikali itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba, na kufafanua kuwa fungu la fedha litaongezwa maradufu ili kuwafikia wale ambao bado hawajapata huduma hizo.
Akizungumzia suala la uvuvi haramu, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaweka uwiano kati ya uhifadhi wa bahari na ustawi wa wananchi wanaotegemea bahari kwa kipato chao.