Dkt. Mabula ataka viwanja vinavyomilikiwa na CCM kutambuliwa kisheria

0
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza na wanachama wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam alipotembelea ofisi za chama hicho. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ubungo Rogert Mbowe.

Na Munir Shemweta

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambaye ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka viongozi wa Chama hicho wilaya ya Ubungo kuhakikisha viwanja vya chama hicho vinatambulika kisheria kwa kuwa na hatimiliki ili kuepuka uvamizi au kuibiwa maeneo ya chama.

Dkt Mabula alisema hayo wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam alipotembelea ofisi za CCM wilayani humo kwa lengo la kusalimia ikiwa ni siku chache baada ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

“Ni lazima chama kisimame kiuchumi kwa kuhakikisha viwanja vitambulika kisheria kwa kuwa na hatimiliki na kama kuna nafasi chama kiweke mipango vizuri ikiwemo ya ubia.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, CCM inavyo viwanja vingi kwenye maeneo mbalimbali nchini, lakini baadhi yake haviko kisheria ingawa vinatambulika kama mali ya chama na kubainisha kuwa kutotambulika kisheria kumepitwa na wakati na kikubwa ni kujua namna uendelezaji rasilimali za chama unavyofanyika. 

“Kama kuna viwanja basi iwekwe mipango vizuri na ikiwezekana kuingia ubia na taasisi kwa ajili ya kuendekeza, Lazima tuangalie maeneo yaliyo katika ‘prime area’. Tusiwe na mawazo tu kuwa hizi ni mali za CCM,” alisema Dkt. Mabula.

Aidha, Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa alikipongeza Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ubungo  kwa kuwa na eneo lake Kibamba Dar es Salaam na kufanikiwa kujenga ofisi ya chama ambapo aliuelezea uamuzi huo kuwa, unakisaidia chama kuepukana na utaratibu wa kupangisha ofisi.

Aidha, aliwataka wanachama wa chama cha Mapinduzi wilaya ya Ubungo kufanya kazi kwa bidii na kuishauri serikali kutimiza majukumu yake ambapo alisisitiza kuwa hayo yote yakitimizwa basi wataweza kuiunganisha serikali na chama na kuongea lugha moja. 

“Kubwa tufanye kazi kwa bidii na kuishauri serikali na kikubwa kutimiza majukumu kupitia ngazi mbalimbali za chama kuanzia shina na tukiweza kuyasimamia  hayo ni jambo la msingi na tutakuwa tumeunganisha chama na serikali vizuri na tutakuwa tunaongea lugha moja, kikubwa kuhakikisha utekelezaji wa ilani kama ilivyokusudiwa,” alisema Dkt. Mabula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here