DAWASA watakiwa kuongeza kasi ya usambazaji maji Dar na Pwani

0

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ametembelea mitambo ya uzalishaji maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini mkoani Pwani, na kuitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuongeza kasi ya usambazaji maji ili kuhakikisha huduma hiyo muhimu inawafikia wananchi wote kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Mwajuma aliambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, pamoja na Menejimenti ya Mamlaka hiyo. Lengo kuu la ziara lilikuwa ni kufuatilia hali ya uzalishaji wa maji na hatua za usambazaji katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani.

Baada ya kukagua mitambo na kujionea shughuli za uzalishaji zikifanyika kwa ufanisi mkubwa, huku kukiwa na upatikanaji wa maji ya kutosha, Mhandisi Mwajuma meiipongeza DAWASA kwa jitihada inazoendelea kufanya katika kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Hata hivyo, ameitaka kuimarisha zaidi kasi ya usambazaji wa maji hayo hadi kufikia ngazi ya mwisho ya mtumiaji.

“Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miradi ya maji, hasa hapa Dar es Salaam na Pwani. Sasa ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na uwekezaji huu. Maji yasibaki kwenye mitambo; yasambazwe kwa kasi ili yawafikie wananchi wote kwa haraka,” Mhandisi Mwajuma amesisitiza.

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka kipaumbele katika Sekta ya Maji kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya majisafi, salama na ya uhakika karibu na makazi yake.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amemshukuru Katibu Mkuu Mwajuma kwa ziara hiyo na kueleza kuwa Mamlaka inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mtandao wa usambazaji maji, ikiwemo kuongeza miundombinu na kufikisha huduma kwa maeneo mapya yanayokua kwa kasi katika jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here