DAWASA watakiwa kumaliza mradi wa maji Kisarawe II

0

Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kumaliza kwa haraka mradi wa maji wa Kisarawe II uliopo Kigamboni, ili kupunguza makali ya ukosefu wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam pamoja na Pwani.

Makalla alisema hayo alipotembelea na kujua hali ya uzalishaji maji akiwa na Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Bodi ya DAWASA, ambapo alisema mradi huo ni muhimu ikizingatiwa kwamba, kina cha maji kwenye vyanzo vya uzalishaji wa maji kimeshuka kwa maana hiyo kutakuwa na upungufu wa maji kwa kiasi kikubwa kwa Mikoa hiyo.

Pia, Mkuu wa Mkoa alisema, Serikali pamoja na Bodi ya DAWASA wamefanya jitihada za upatikanaji wa maji, hivyo aliwataka wananchi kutumia vizuri nishati hiyo pale inapopatikana.

Aidha, alisema Kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro zimetimiza majukumu yake kwa wale wote wanaochepusha maji, ambapo hatua zimechukuliwa ili kuhakikisha hakuna hujuma zinazofanyika na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwenye Mto Ruvu.

“Hakuna kisingizio kingine chochote cha kina cha maji zaidi ya utegemezi wa mvua na hapa nasisitiza kuwa, Serikali inafanya jitihada kwa hiki kidogo kilichopo kinawafikia wananchi na asije mtu akasema hata mvua inaweza kuletwa na Serikali,” alisema Makalla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here