CHAN kukuza uchumi, kuinua vijana na kuutangaza utalii wa Z’bar

0

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema mashindano ya Ligi za Ndani za Mataifa (CHAN 2024) yatafungua fursa pana za kukuza uchumi, kuinua vijana, na kuutangaza utalii wa Zanzibar kitaifa na kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa New Amaan Complex, Waziri Tabia amesema maandalizi ya mashindano hayo yamefikia hatua nzuri na yamezingatia vigezo vyote vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa ni pamoja na viwanja, miundombinu ya malazi, usafiri, ulinzi, huduma za afya na maeneo ya mazoezi.

“Mashindano haya yatasaidia kuongeza shughuli za biashara, kuzalisha ajira na kuimarisha mshikamano baina ya nchi shiriki. Ni fursa muhimu kwa vijana wetu na taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Tabia.

Ameongeza kuwa, kutokana na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini, wageni watakaofika Zanzibar watapata fursa si tu ya kufurahia burudani ya soka bali pia kuonja utamaduni, ukarimu na uzuri wa Zanzibar.

Aidha, Waziri Tabia ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa dhamira yao ya dhati ya kuimarisha viwanja vya michezo na kukuza sekta ya michezo nchini.

Waziri amewashukuru waandishi wa habari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa weledi, na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa michuano hiyo ili kutoa hamasa kwa timu shiriki.

Kwa mujibu wa ratiba, mashindano ya CHAN kwa Tanzania Bara (Kundi B) yanatarajiwa kuanza Agosti 2, 2025, yakizihusisha nchi za Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa upande wa Zanzibar (Kundi D), mechi zitaanza Agosti 5, 2025 na timu zitakazoshiriki ni Senegal, Nigeria, Congo na Sudan.

Jumla ya timu 19 kutoka nchi mbalimbali zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo makubwa ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa nchi tatu: Kenya, Uganda na Tanzania chini ya kaulimbiu: “Kama si sasa, ni sasa hivi!”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here