Na Fred Kibano
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa kulinda amani ya wananchi na kuwa waadilifu katika utendaji wao.
Chalamila ametoa kauli hiyo mapema hivi karibuni wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa hao ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Kumekuwa na tatizo la uvunjifu wa amani mkubwa kwenye maeneo yetu, hii kitu ipo kwenye makata yetu, ni vizuri sana leo watendaji mtajengewa uwezo kuangaliani ni vipi hasa mnawajibika kwenye maeneo yetu” alisema Chalamila.
Aidha, Chalamila amewataka watendaji hao kuwajibika kwa wananchi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma, kulinda amani, kutatua kero na migogoro, na pia kukagua miradi ya maendeleo kwa weledi kwenye maeneo yao hali wakizingatia kuwa kiungo kizuri kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Ametolea mfano wa kero ya kuwepo kwa madanguro Jijini Dar es Salaam na kusema biashara hiyo haramu imekuwa ikiwaingizia fedha watu wachache kwa wastani wa Milioni 21.5 kwa mwezi kwa kila danguro, lakini madhara yake ni makubwa miongoni mwa jamii na hapo wao wanatakiwa kuwa wa kwanza kupata taarifa na sio mpaka Viongozi wa juu watambue au kuambiwa tatizo lililopo kwenye eneo lao.
Akitoa neno kabla ya hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda alisema, mafunzo hayo ni msaada mkubwa hasa kutokana na kukua kwa teknolojia, lakini pia ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu.
Naye Ibrahim Minja Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa alisema, malengo ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo katika majukumu yao kwani watatambua umuhimu wao kama kiungo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vile kukagua miradi ya maendeleo kwa thamani ya fedha halisi.