Na Mwandishi Wetu, Kilosa
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amevunja ukimya baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuyafuta umiliki mashamba makubwa yenye ekari 23,016 katika halmshauri za wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro na kisha kuyagawa kwa wananchi, baada ya wawekezaji wake kushindwa kuyaendeleza.
Akizungumza wakati akizindua msimu wa kilimo kwa Mkoa wa Morogoro, wilayani Kilosa, Shaka alisema ufutaji wa mashamba hayo haukufanywa kwa bahati mbaya au kwa kubahatisha bali ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 20202-2025.
“Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi tumezungumza vizuri sana, ukisoma Ibara ya 74 tumezungumza vizuri namna ya kuhuisha na kuboresha matumizi bora ya ardhi, lakini tumezungumza namna ya kufuta mashamba ambayo kwa muda mrefu kuna watu walijimilikisha na wakayatelekeza.
“Lakini mashamba ambayo wajanja wajanja waliamua kuyachukua kwa njia moja au nyingine ili kukwamisha shughuli za maendeleo. Bahati nzuri nimewahi kuwa Katibu wa CCM katika Mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha miaka miwili.
“Nilipofika kwenye mkoa huu kwa kipindi cha miezi sita sikukaa ofisini nilikuwa nakuja na kurudi Kilosa asubuhi na jioni. Kazi moja kubwa ambayo niilifanya kwa ustadi mkubwa ni kupokea malalamiko ya ardhi, nadhani kwenye Mkoa wa Morogoro na hasa Kilosa ilikuwa inaongoza kwa malalamiko ya ardhi. Kesi kubwa za wilaya hii wako watu wamejimilikisha mashamba na hayaendelezwi,” alisema.
Aliongeza kuwa, wako wajanja wamechukua mashamba ya wenzao lakini hakuna kinachofanyika, lakini kesi kubwa ya Kilosa ilikuwa ni namna ambavyo hakukua na mpango bora wa matumizi ya ardhi ndani ya wilaya hiyo.
“Kwa mtazamo wangu kwa sababu sisi tulifanya kazi kubwa sana na tulifanya kazi ngumu kweli kweli, kwa maoni yangu viongozi mlioko kwenye mkoa huu mmeanza vizuri,” alisema.
Shaka alisema, Rais Samia tangu ameingia madarakani ameweka mkazo na msisitizo katika kilimo na ndio maana wote ni mashahidi kwani ameongeza bajeti ya kilimo kwa kiasi kubwa kutoka Shilingi Bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi Bilioni 954 mwaka 2022/2023.
“Hiyo haijapata kutokea tangu tumepata uhuru kwenye bajeti ya kilimo yenye fedha nyingi kama hii. Tafsiri yake tunakwenda kutafsiri kwa vitendo kilimo ndio uti wa mgongo lakini kilimo ndio mkombozi kwa maendeleo ya nchi yetu.
“Rai yangu vijana hawa lazima wawezeshwe kwa mitaji, vijana lazima wawekewe utaratibu mzuri wa kusimamiwa na tuhakikishe wanaendelea sio wanarudi nyuma,” alisema.
Shaka aliongeza kuwa, ni vema madiwani na viongozi wengine kwenye ngazi ya halmashauri kuhakikisha wanasimamia fedha zinazotolewa kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha zinafika kwa walengwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amefuta mashamba makubwa 14 yenye ukubwa wa ekari 23,016 katika Halmashauri za Mvomero na Kilosa ili yagawiwe kwa wananchi jambo ambalo limeelezwa ni heshima kubwa kwa wananchi.
Mwasa alisema, mashamba hayo yameanza kugawanywa kwa wananchi kwa mfumo wa Block Farming ili kuongeza ufanisi zaidi.