Na Mwandishi wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyetoa wito muhimu unaowataka watanzania wote kulinda na kutunza Amani ya Taifa lao.
Vile vile, CCM kimewashauri watanzania kuanza na kutafakari hatimaye kutekeleza ushauri huo uliotolewa na Mkuu wa nchi na kuufanyia kazi.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, aliyesema wananchi si kwamba wanapaswa kuutafakari tu, lakini pia wautekeleze wito huo wa Rais Dkt. Samia.
Mbeto alisema, tunu ya Amani ni jambo mtambuka kwa kila nchi duniani, hivyo si vyema wananchi wakawa tayari kufuata mkumbo kwa kujiingiza katika ushabiki wa kuvuruga Amani na utulivu.
Alisema, Mataifa mengi yaliyopoteza Amani, Utulivu na Umoja, wananchi wake ndio wanaoshi katika maisha ya magumu yenye shida, wakikabiliwa na njaa, kukosa mahitaji muhimu, huku wakisakamwa kwa maradhi na unyonge bila kupata matibabu.
“Kwa kauli moja CCM tunaipongeza hotuba ya Rais Dkt. Samia aliyoitoa kwenye Baraza la Idd El Fitry unaowataka watanzania kulinda, kusimamia na kuitunza Amani ya Taifa lao. Kupotea kwa Amani kuna mshikemshike mkubwa na majuto,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliwataka viongozi wa Kiimani, wa Kijamii, Wanasiasa na makundi mengine kuwa mstari wa mbele kuutekeleza wito wa Amani uliotolewa na Rais ukimtaka kila mwananchi kutovuruga Amani.
“Tunampongeza Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu kwa kutoa wito huu muhimu mapema kuelekea Oktoba mwaka huu. Kuthubutu kuchezea Amani ya nchi hatari yake ni sawa na mtu anayechezea transfoma la umeme wa gridi ya Taifa,” alisema.
Pia, Mbeto aliwaasa wanasiasa wenzake kujua umuhimu wa rasilimali ya Amani ilivyo na umuhimu wa kipekee katika jamii, hivyo akawataka wachunge ndimi zao wanapokuwa kwenye majukwaa ya kisiasa.
“Ulimi ni nyama ndogo laini ndani ya mdomo wa binadamu. Ulimi huo unahitaji kuchungwa wakati wote. Neno dogo lisilo na tahadhari huzusha majanga yasiozuilika. Neno baya ni kama cheche ya moto inapodondokea nyasi kavu,” alisisitiza Mbeto.
Hata hivyo, CCM kimewataka viongozi wa CCM kwenye ngazi zote za chama, kuendelea na kuwa mfano mzuri katika jamii kwa kutotamka matamshi yanayoweza kukipaka matope chama hicho.
“Kiongozi, kada au mwanachama yeyote mkereketwa wa CCM ambaye ataropoka na kutoa matamshi yanayotishia kuvuruga Amani, hatua kali za kinidhamu na kimaadili zitamhusu. Kila anayetaka kusema kwanza ayapime maneno yake. Amani si kitu cha mzaha cha kukichezeachezea ” alieleza Katibu huyo.