CCM walaani tangazo batili la ACT Wazalendo

0

📌 Wahoji wanapata wapi Mamlaka ya kuiingilia ZEC?

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WAKATI uandikishaji wapiga kura ukimalizika salama Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM ) kimehoji ni wapi ACT-Wazalendo kinakopata Mamlaka ya kuingilia na kufanyakazi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kutangaza Takwimu za Uandikishaji.

CCM kimelaani tangazo batili lilitangazwa na Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo, Omar Ali Shehe na kuitaja ina lengo la kuijengea jamii hofu na wasiwasi.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, alisema hatua ya kiongozi huyo kujibebesha kazi za ZEC, ni mwanzo wa utata na ukorofi.

Mbeto alisema, kitendo chake cha kutoa taarifa na takwimu za uandikishaji wakati yeye si Mtendaji wala Afisa dhamana wa ZEC, huku Tume haijatamka lolote, ni wazi ACT kinatafuta hekaheka.

Alisema, wananchi wa Zanzibar hawataki kuingizwa kwenye msitu wa hekaheka, purukushani na mivutano isiyo na ulazima kwa kisingizio cha uandikishaji kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu.

“Omar Ali Shehe amekuwa akiutumia vibaya uhuru wa kisiasa na demokrasia iliopo Zanzibar. Anaandaa mazingira tele yenye kiza kinene. ZEC ina wajibu wa kuchukua hatua za haraka kwa Mujibu wa Sheria ya uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018 kifungu 128(b),” alisema Mbeto.

Aidha, alisema katika kifungu (b), kinakataza mtu kuingilia majukumu, mamlaka na uhuru wa Tume kwa kutoa taarifa au kuagiza kutoa taarifa juu ya jambo lolote ambalo lipo chini ya Mamlaka ya Tume.

“Omar Shehe amepata wapi nguvu hizo . Amepewa na nani kazi au mamlaka ya kuingilia kazi za ZEC . Kwa makusudi anajaribu kutaka kuiburuza ZEC. Atimize majukumu yake ya kisiasa akiwa ACT, ZEC ni chombo kinachojitegemea,” alisema Mbeto.

Kadhalika kifungu hicho kinamtaja mtu atakayefanya kosa hilo, akipatikana na hatia, atalipa faini isiyopungua Shilingi laki mbili, isiyozidi Shilingi Milioni tano au atatumikia kifungo kisichopungua miezi sita, kisichozidi mwaka mmoja au adhabu zote.

“Tunaitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuhakiksha Sheria inachukua mkondo wake. Kufumba macho au kupuuzia ni kuruhusu uvunjifu wa sheria nyingine zilizopo,” alieleza.

Mbeto alisema, mara kadhaa amekuwa akimtaja Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Omar Shehe ni mtu kiherehere, anayetamani siasa za mikikimiki ambazo zikitokea hatazihimili.

“Tumejenga nchi ya kidemokrasia inayoheshimu misingi ya haki, utu na Sheria. Tunaishauri Tume ichukue hatua dhidi ya kitendo hiki kiovu cha uvunjifu wa sheria na kukikomesha ili kiisijirudie tena”

Mbeto alisema, hatua ya Shehe kutaja takwimu za uandikishaji na idadi ya Wapiga kura 99,723, kwa kuitaja Pemba imeandikisha wapiga kura 26,515 na Unguja 73,212 , hizo ni takwimu za ACT kwani ZEC bado haijatangaza lolote.

“Wakati wa uandikishaji Maafisa wa CCM wamepita vituo vyote Unguja na Pemba. Vituo vingi vimekutwa havina mawakala wa ACT. Ni ajabu Omar Shehe anaposoma takwimu za ubashiri na unajimu,” alisema Mbeto.

Vile vile, Mbeto alisema maeneo mengine ambayo ACT hakikuweka mawakala ni Zingwezingwe, Kiongwe Kidogo, Kijibwe Mtu na Donge Vijibweni ambapo awamu ya kwanza ya Iandikishaji ,Vituo takriban 56, ACT hakikuwemo mawakala wake ikiwemo shehia ya Mitiulaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here