CCM: Tumejiandaa kushinda 2025

0

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanachama wake kutambua, Uchaguzi Mkuu si jambo la dharura na ghafla, hivyo kila mmoja ajue wakati umefika wa kusimama pamoja kutafuta ushindi wa chama.

Pia, chama hicho kimewahimiza wanachama wake wote, kujitokeza itakapoanza ngwe za kampeni na siku ya upigaji kura, kwani uchaguzi ni suala la kufa na kupona.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ametoa maelezo hayo huku akiwataka wanachama wote kushiriki kwa nguvu zote kuwachagua wagombea toka CCM.

Mbeto alisema, ni muhimu kwa kila mwanachama wa CCM ajue kuwa kujitokeza kwao siku ya kupiga kura, wajione wamebeba urithi wa wazazi unaotokana na vyama vya TANU na ASP vilivyoleta Uhuru na mapinduzi.

Alisema, uchaguzi ndio unaoviweka vyama vya siasa madarakani, hivyo anawahimiza wananchi wa Tanzania na Zanzibar, kwenda kuwapigia kura wagombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

“Uchaguzi si jambo na zoezi la ghafla. Kila baada ya miaka mitano hufanyika. Pamoja na CCM kuionyesha dunia nchi zetu zinaongozwa kidemokrasia. Matumaini yote ya wananchi yamebebwa na sera za CCM si vinginevyo,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, kipimo cha kuchaguliwa tena Rais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi kinatokana na ufanisi wa kazi kubwa walizozifanya miaka mitano iliopita.

“CCM kinashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025/2030 kikiwa na matumaini makubwa ya kushinda kuliko miaka yote. Kitashinda kwani kimetimiza wajibu na ahadi zake kwa jamii na kwa maendeleo ya nchi,” alisema Mbeto.

Alisema, kutokana na kufanyika kazi kubwa iliyotokana na utendaji wenye ufanisi na utekelezaji wa kisera, CCM kitashiriki uchaguzi huo Oktoba kwa lengo moja tu la kushinda na kuongoza dola.

“Tumetekeleza ahadi zetu zote kama chama tawala. Marais wetu wametoka jasho na kutimiza wajibu kwa vitendo na utumishi uliotukuka. Kazi iliobaki ipo kwa wananchi wanaosubiri kutia tiki katika karatasi za kura,” alieleza.

Hata hivyo, Katibu huyo mwenezi alisema, CCM lazima ishinde kwakuwa kinaaminiwa na wananchi walio wengi, kina viongozi wazalendo, sera makini na Siasa safi.

“Chama chetu hakisubiri kudandia au kuvizia wagombea wanaotemwa na vyama vingine ili wagombee urais na ubunge. Tuna mamia ya wagombea madhubuti wanaoeleweka na wazalendo wasiotiliwa shaka yoyote,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here