CCM: Rais Dkt. Samia ametushangaza

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina kila sababu ya kujivunia utekelezaji wa sera zake kutokana na utendaji kabambe wa miaka minne chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tokea ashike urais na kukishangaza chama hicho.

Pia, chama hicho kimetaja baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Serikali ya Awamu ya sita, imekwenda sambamba na ahadi katika ilani ya chama hicho, kisera, kwa uwazi uwajibikaji na umakini.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, alipozungumza na Waandishi vyombo vya habari katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Mbeto alisema, dhamana ya uongozi wa nchi ni zaidi ya mzigo mzito, anapobebeshwa mwenzenu ili aubebe kwa kichwa mwake huku mkimtazama jinsi atakavyosimamia dhamana hiyo kuifanikisha kwa ufanisi.

Alisema, kutokana na uwezo binafsi alionao Rais Dkt. Samia, Wasaidizi wake, Washauri wake, Wataalam, Baraza lake la Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya hadi Watendaji Kata na Vijiji, amefanikisha kwa viwango vya utelekezaji ulioleta tija kimaendeleo.

“Kwa upande wetu CCM tuna sababu zote za kujivunia kazi ilioleta ufanisi kwa nchi chini ya usimamizi wa serikali ya awamu ya sita. Rais Dkt.Samia ametimiza wajibu wake wa kusimamia majukumu aliopewa na wananchi,” alisema Mbeto.

Aidha, alisema wakati akishika urais, kuna baadhi ya watu walijiuliza itakuwaje kwa Rais wa kwanza mwanamke atakavyofanya kazi zake. Kwa kujiamini kwake, Rais Dkt. Samia ametimiza majukumu yote ya kiuongozi, kisera na kiutawala bila kuyumba. Wapo pia waliotaka kumuona atakavyokamiliisha miradi mikubwa ya kimkakati.

“Kwa bahati nzuri miradi yote ya kisera ilioanzishwa awamu ya tano, imekamilika kwa kiwango cha juu. Katika Awamu ya tano, Rais Dkt.Samia alikuwa Makamo wa Rais, chini ya Hayati Rais Dkt. John Magufuli. Alihusika katika kupanga na jinsi ya utekelezaji wake utakavyokamilika,” alieleza

Katibu huyo Mwenezi alisema, licha ya Rais Dkt.Samia kusimamia wajibu huo wa kiutendaji, Serikali yake, amepata heshima kubwa katika medani za diplomasia Kimataifa, huku Tanzania chini utawala wake, ukiendelea kuaminiwa na Taasisi za Fedha za Kimataifa, Benki ya Dunia, Nchi Washirika wa Maendeleo na Shirika la Fedha la Kimataifa.

“Dunia ya leo ni ndogo kuliko kitongoji kimoja. Kiongozi atakayejifungia Ikulu kutwa kucha. Akijisahau tu dunia itamtenga, mabadiliko muhimu yatampita. Rais Dkt. Samia hakusita kutoka, kusafiri na kushiriki kwenye majukwaa ya Kimataifa,”alisisitiza.

Mbeto aliongeza kusema, licha ya Serikali ya CCM kukamilisha miradi kadhaa ya kimkakati ilioainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM Mwaka 2020-2025, hata miradi ilioanzishwa na Awamu ya sita, pia imekamilika kwa wakati uliokusudiwa.

“Ndiyo maana CCM kinatembea kifua mbele ikijivunia uongozi wa Mama. Tunachokihimiza toka sasa kuelekea 2030 Kazi na Utu tunazidi kusongambele. Kila mtu aheshimu Utu wa mwenzake, afanye kazi, azalishe kwa bidii, Taifa lifikie kilele cha Maendeleo,” alisema Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here