CCM: Mapokezi ya Dkt. Mwinyi yamekata ngebe za Jussa

0

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kujitokeza kwa mamia ya watu Zanzibar, kumpokea Makamu Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kumekata ngebe za Makamu Mwenyekiti wa ACT Ismail Jussa Ladhu.

Chama hicho tawala pia kimemtaka Jussa kutokulinganisha ACT na CCM, kwani vyama hivyo havifanani kisera, kihistoria, kiuchumi na kisiasa.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi tikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, wakati akihojiwa na waandishi wa Habari katika Afisi za CCM Zanzibar hapo Kisiwandu.

Mbeto alisema, si kisiasa, kimfumo na kimuundo, ACT Wazalendo hakiwezi kujifananisha na CCM ambacho kimekomaa katika uongozi bora, kina viongozi makini wenye uzoefu na ufahamu wa mambo ya diplomasia, utawala na siasa.

Alisema, CCM kilikuwa kikipata mikwaruzo ya hapa na pale ya kisiasa wakati wa viongozi walifukuzwa toka CCM wakaunda CU, lakini si safu ya ACT chini ya uongozi wa Othman Masoud Othman na mwenzake Jussa.

Alisema, CCM kiliumizwa kichwa na safu ya wanasiasa waliokulia na kukomazwa kisiasa na CCM; Maalim Seif Sharif Hamad, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu na Hamad Rashid Mohamed.

“Viongozi wengine waliotupa tabu kidogo ni Mohamed Dedes, Machano Khamis Ali, Khatib Hassan Khatib na Soud Yusuf Mgeni. Sio hawa kina Othman, Jussa, Salum Bimani au Omar Ali Shehe. Hawa ni cha mtoto. Hawawashi wala hawazimi” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema kujitokeza mamia ya wananchi, waliomlaki Rais wa Zanzibar Dkt. Mwinyi ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar, mapokezi yake yameacha gumzo na simulizi kila kona.

“Hatuna hofu ya kushinda ifikapo Oktoba Mwaka huu .Tutashinda kutokana na utendaji makini wa SMZ. Utekelezaji wa sera ,ufanisi wa kiutendaji na ukamilishaji miradi ya kisekta. Ahadi hadi zetu za kisera kwa wakati sahihi,” alieleza Mbeto.

Hata hivyo, Katibu huyo alisema zama za kuwadanganya wananchi na kuwapa matumaini yasiotekelezwa, zimepitwa na wakati badala yake kizazi kipya kinahitaji kujionea juhudi za maendeleo kwa vitendo.

“Kama Mwanasiasa mmoja aliahidi atajenga uchumi wa Zanzibar kwa siku mia moja. Ajabu kuna walioamini wakati jambo hilo haliwezekani. Ni ahadi za kiabunuwasi na Simulizi za Alifu Lelaulela. Anahitajika mgombea kama Rais Dkt. Mwinyi,” alisisitiza.

Mbeto aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuwa watulivu, walinde Amani, Umoja ,Upendo na Mshikamano kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.

Mbeto alisisitiza miaka mitano ijayo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi, Zanzibar itatimiza ndoto yake ya kuwa Dubai, Malaysia au Hong Kong ya Afrika Mashariki kwa maendeleo yatakayoishangaza dunia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here